Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

ONGEZENI UBUNIFU KATIKA HUDUMA MPYA MNAZOTOA

Posted on: September 20th, 2024

Na WAF - Mbeya

Serikali imewataka Waganga Wafawidhi wa Hospitali za rufaa za mikoa Tanzania Bara kuongeza Ubunifu na kuanzisha huduma mpya za Kibingwa katika hospitali zao ili wananchi wapate huduma bora za afya.

Wito huo umetolewa na Dkt Nyembea Septemba 20, 2024 jijini Mbeya wakati akihitimisha kikao kazi cha Waganga Wafawidhi, Wauguzi Wafawidhi, Makatibu wa Hospitali na Waratibu wa Ubora wa Huduma(QI) wa Hospitali za Rufaa za mikoa ya Tanzania bara.

"Kupitia kikao hiki hakikisheni mnakwenda kuboresha huduma na kuanzisha angalau huduma mpya za kubingwa nane kwenye Hospitali zenu ili kuendelea kuongeza imani kwa wananchi."

Mbali ya Ubora wa huduma Dkt. Nyembea amewataka wafawidhi kuboresha stahiki za madaktari Bingwa ili madaktari hao wasifikirie kuhama (retantion) kwa kuwawekea mazingira wezeshi yatakayonfanya Daktari Bingwa abaki kwenye Kituo chake,

"Kama wizara tumejiwekea malengo kuwa ifikapo mwaka 2026 huduma nane za kibingwa katika hospitali zote za rufaa za mikoa ikiwemo huduma za utengemao ziwe zimeanza kutolewa, ambapo mpaka mpaka sasa ni hospitali saba ambazo zinatoa huduma za utengema."

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Waganga wafawidhi Dkt. Bahati Msaki ambae ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya mkoa wa Mwanza Sekotoure, amewashukuru viongozi wa Wizara ya Afya kwa kufanikisha kikao hicho kwani kimekuwa na tija kwa mustakali wa afya za watanzania huku akiahidi kuendelea kuboreshwa kwa huduma hizo.