MIAKA MINNE YA RAIS SAMIA WATU ZAIDI YA LAKI TISA WAPATIWA HUDUMA BMH
Posted on: March 4th, 2025
Na WAF – Dodoma
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imetoa huduma za matibabu kwa watu 970,000 katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamebainishwa leo Machi 04, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi, wakati akiwasilisha taarifa ya mafanikio ya Hospitali ya Benjamin mkapa mkoani Dodoma.
Prof. Makubi amesema hospitali imeendelea kuimarisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi ili kuboresha afya za Watanzania.
“Tumefanikisha upandikizaji wa figo kwa wagonjwa 250, huku wagonjwa wengine 10 wakinufaika na huduma hii kupitia mfuko maalumu wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Dkt. Makubi.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali imetumia kiasi cha Shilingi Bilioni 1.4 kutoka katika Mfuko Maalum wa Rais wa Jamhurinya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa selimundu.
Katika kuboresha huduma za uchunguzi na matibabu ya mfumo wa chakula, hospitali imeongeza vifaa tiba vya kisasa na kusomesha wataalam, hali inayochochea kuhudumia zaidi ya wagonjwa 10,000 katika eneo hilo.
“BMH pia imeanzisha huduma za mkoba kwa kusambaza madaktari na wataalam wa afya katika mikoa mbalimbali ambayo haina huduma za kibingwa na kibingwa bobezi, hatua inayolenga kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya popote walipo,” amesema Dkt. Makubi.
Prof. Makubi amesema hospitali imepanua huduma zake hadi kimataifa kwa kutoa huduma za matibabu kwa wageni kutoka nchi mbalimbali.
Aidha, Prof. Makubi amesema hospitali hiyo inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi ili kuboresha zaidi huduma zake kwa wananchi na kuifanya kuwa kituo cha rufaa cha mfano katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kuhusu vifaa Prof. Makubi amesema wameongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kutoka asilimia 68 mwaka 2022 na kufikia asilimia 96 mwaka 2025, kutokana na kuongeza kwa bajeti ya dawa pamoja na Serikali na kufungua vituo vya dawa katika hospitali.