Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI 9 WAKUTWA NA HATIA KUFUATIA UVUNJIFU WA MAADILI YA KITAALUMA

Posted on: February 9th, 2024


Na. WAF - Dar Es Salaam


Baraza la Madaktari Tanganyika limewatia hatiani na kuwapa adhabu madaktari Tisa kwa makosa ya ukiukwaji wa kanuni za maadili na utendaji wa kitaaluma na kutoa maamuzi dhidi ya wanataaluma hao kupitia Kikao cha Baraza la Madaktari Tanganyika kilichokaa kati ya tarehe 22 hadi 26 Januari 2024 lililosikiliza jumla ya mashauri Tisa. 


Hayo yamebainishwa leo Februari 9, 2024 na Mwenyekiti Baraza la Madaktari Tanganyika Prof. David Ngassapa akiwa anazungumza na waandishi wa habari kuhusu mashauri ya Kitaaluma yaliyowasilishwa mbele ya Baraza hilo Januari 2024. 


Miongoni mwa adhabu zilizotolewa ni pamoja na kufutiwa usajili, kufungiwa leseni ya kutoa huduma kwa muda kati ya miezi sita hadi wa miaka Miwili, kupewa onyo au karipio kali na pia walielekezwa kwenda kwenye mafunzo ya weledi, maadili ya kitaaluma na huduma kwa mteja ya Wizara ya Afya kwa muda wa miezi sita kwa gharama zao.


Aidha, Mwenyekiti Prof. ngassapa amesema Baraza linatoa rai kwa wanataaluma wote nchini kuzingatia Kanuni na maadili ya kitaaluma za mwaka 2005 na kufuata miongozo ya utoaji huduma kwa lengo la kulinda Afya ya Mgonjwa.


Baraza limebaini pia baada ya mapitio ya mashauri mbalimbali kuwa maeneo mengi ya misingi ya maadaili ya kitaaluma yameonekana kutokutiliwa maanani na wanataaluma kwenye kutoa huduma za Afya kwa wagonjwa.


“Hivyo, Baraza linaelekeza kuzingatiwa kwa misingi ya maadili wakati wa kutoa huduma ikiwemo kujaza fomu za ridhaa ya huduma (informed Consent) kwa mgonjwa, kumuelimisha mgonjwa madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa matibabu na kuwa kushindwa kufuata hayo, watakuwa wameenda kinyume na Sheria ya Udaktari, Udaktari wa Meno na Afya Shirikishi Sura Na. 152 pamoja na kanuni zake.