Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA YAIMARISHA UTAYARI WA WATUMISHI WA AFYA RUVUMA KUKABILIANA NA UGONJWA WA EBOLA

Posted on: November 7th, 2026

Na Happyness Hans, WAF - Ruvuma

Mkurugenzi wa Huduma za Dharura na Maafa kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Michael Kiremeji, amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani WHO imeimarisha utayari wa watumishi wa afya mkoani Ruvuma kupitia mafunzo ya vitendo na tathmini ya vituo vya kutolea huduma za afya, kwa lengo la kujiandaa kukabiliana na magonjwa ya milipuko, hususan Ebola.

Akizungumza leo Novemba 7, 2026 mkoani Ruvuma, wakati wa kuhitimisha ziara ya timu ya wataalamu mkoani humo, Dkt. Kiremeji amesema timu imefanya tathmini katika vituo mbalimbali vya afya karibu katika halmashauri zote za mkoa huo, ikiwemo Hospitali za Peramiho, Nyasa, Mbinga, Songea RRH pamoja na hospitali nyingine za binafsi, ili kubaini na kuimarisha utayari wa kukabiliana na ugonjwa huo.

Amesema baadhi ya nchi za Afrika zimeanza kuripoti maambukizi ya Ebola, hivyo Serikali imeona umuhimu wa kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya mkoani Ruvuma ili waweze kujikinga wanapomhudumia mgonjwa, pamoja na kuzuia uwezekano wa kusambaza maambukizi kwa watu wengine. Jumla ya watumishi zaidi ya 90 wamepatiwa mafunzo hayo ya vitendo.

Kwa upande wake Mratibu wa huduma za dharura na magonjwa ya milipuko mkoa, Dkt. Yona Mwakabumbe, akizungumza kwa niaba ya uongozi wa mkoa, ameishukuru Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kutoa mafunzo hayo yaliyolenga kujenga uwezo wa watumishi wa afya kukabiliana na Ebola. Amesema timu hiyo imekuwa mkoani humo tangu Novemba 2, 2026, hatua itakayosaidia kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema yamewajengea uelewa kuhusu njia sahihi za kujikinga wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa, kuzuia maambukizi na kuhakikisha hawawi chanzo cha kusambaza ugonjwa kwa watu wengine. Wameeleza kuwa maarifa na ujuzi walioupata vimeongeza utayari wao wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko, hususan Ebola.

Aidha, washiriki hao wameeleza umuhimu wa kuendelea kuimarisha maandalizi ya maeneo maalumu ya kuwahudumia wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na Ebola