Wizara Ya Afya

TANZANIA YAENDELEA KUJIZATITI KUKABILIANA NA UGONJWA WA EBOLA

Posted on: November 7th, 2026

Kikosi kazi kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kimefanya ziara ya kukagua maeneo ya mipaka kati ya Kenya na Tanzania ya Sirari na Kirongwe iliyopo katika Mkoa wa Mara ili kuona hali ya utayari wa nchi katika kukabiliana na ugonjwa wa Ebola uliotangazwa kuingia nchini Kenya.

Ziara hiyo inayoongozwa na Mkurugenzi wa huduma za dharura na maafa Dkt. Erasto Sylvanus kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali imetembelea mipaka hiyo ili kukagua utayari wa sehemu ya afya (Port Health) namna ilivyojipanga kufanya uchunguzi wa afya kwa wasafiri na wageni wanaoingia nchini ili kuona namna gani imejipanga endapo atabainika mhisiwa wa Ugonjwa wa Ebola.

Kikosi kazi hicho kimetembelea na kukagua katika maeneo ya kuingia wageni, kuangalia mashine za kupima joto, ujazaji wa fomu za taarifa afya za msafiri pamoja na sehemu ambayo mhisiwa atahifadhiwa endapo atabainika akisubiri kuchukuliwa na kupelekwa Hospitali kwa uchunguzi na matibabu zaidi.

Aidha, kikosi kazi hicho kimeonesha kuridhishwa na utayari uliopo katika mipaka hiyo huku kikitoa ushauri kwa wataalam waliopo katika mipaka hiyo kuendelea kuwa makini katika uchunguzi wa dalili za awali kwa wasafiri wanaoingia ili kuzuia ugonjwa wa Ebola usiingie nchini.

Kabla ya kutembelea mipaka ya Sirari na Kirongwe kikosi kazi hicho kilitembelea uwanja wa ndege wa Musoma pamoja na Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (Kwangwa) ili kuona maaandalizi ya jumla endapo mhisiwa wa Ebola atapatikana kuwa na dalili za ugonjwa wa Ebola