Wizara Ya Afya

MWANANCHI WENYE KADI YA BIMA AHESHIMIWE” — MAELEKEZO YA MCHENGERWA KWA WATOA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: November 5th, 2026

Na Amos Luzuga,WAF- Dodoma

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amewataka wasimamizi wa hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya nchini kuhakikisha wanachama wa mifumo ya bima ya afya wanapokelewa kwa heshima, wanahudumiwa kwa lugha nzuri na kupata huduma kwa wakati huku akisisitiza kuwa hakuna mgonjwa anayepaswa kudhalilishwa au kukatishwa tamaa anapokwenda kutafuta matibabu.

Akizungumza leo, Novemba 5, 2026, katika kikao cha menejimenti na watumishi wote wa Wizara ya Afya kilichofanyika Jijini Dodoma, Mchengerwa amesema mafanikio ya mfumo wa Bima ya Afya yanapaswa kupimwa pia kwa idadi ya wananchi wanaotumia kadi zao kupata huduma, badala ya kujikita katika kiwango cha fedha zinazokusanywa na vituo vya kutolea huduma.

“mtu anapokwenda hospitali hatutegemei tusikie kwenye kituo kuna fedha nyingi, tutegemee kuna kadi nyingi zimetumika. Maana yake, wanaokwenda tunataka wawe na kadi, tunawapatiaje kadi kama watu wako stressed? Mtu anakwenda anaambiwa hiki, anafokewa. lugha lazima zibadilike. Yaani hakuna namna nyingine, ni lazima mwenye kadi aheshimiwe, apokelewe vizuri,” amesema Mchengerwa.

Aidha, amesisitiza kuwa ucheleweshaji wa huduma na changamoto za usimamizi katika hospitali zinapaswa kushughulikiwa kwa vitendo, akiwataka wasimamizi wa vituo kutoka ofisini na kufuatilia moja kwa moja utoaji wa huduma ili kubaini vikwazo vinavyowakabili wagonjwa na kuvipatia ufumbuzi.

Hata hivyo amesema kuwa kuwa mfumo wa NHIF unaweza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi pale ambapo wagonjwa wanapokelewa vizuri, wanahudumiwa kwa wakati.

Maelekezo hayo yanaweka msisitizo katika wajibu wa taasisi za afya kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora unaendana na heshima, utu na haki za wagonjwa, huku utekelezaji wake ukihitaji usimamizi wa karibu na uwajibikaji wa watumishi katika ngazi zote nchini.