WIZARA YA AFYA, TERUMO BCT KUSHIRIKIANA KUIMARISHA HUDUMA ZA SIKOSELI NCHINI
Posted on: November 10th, 2026Wizara ya Afya na Kampuni ya Terumo Blood and Cell Technologies (Terumo BCT) zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU), kwa lengo la kuimarisha huduma za kinga, uchunguzi, matibabu na usimamizi wa ugonjwa wa sikoseli nchini.
Akizungumza leo Novemba 10, 2026 Jijini Dodoma katika Ofisi za Wizara ya Afya Dkt. Eliud Eliakimu Mkurugenzi Uhakiki Ubora Wizara ya Afya kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuimarisha huduma kwa watu wanaoishi na ugonjwa wa sikoseli nchini.
Amesema pamoja na mafanikio yaliyokwisha patikana bado Tanzania inakabiliwa na changamoto ya ugonjwa huo, ambapo takwimu zinaonesha kuwa takribani watoto 14,000 huzaliwa na ugonjwa wa Sikoseli kila mwaka, huku asilimia 15 hadi 20 ya Watanzania wakiwa na vinasaba vya ugonjwa huo.
Aidha, amesema takribani asilimia tano hadi saba ya vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano vinahusishwa na ugonjwa huo, hali inayoonesha umuhimu wa kuimarisha mifumo ya afya katika kukabiliana na Ugonjwa huo.
Dkt. Eliud ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuimarisha huduma za afya, ikiwemo huduma za magonjwa yasiyoambukiza kama sikoseli na magonjwa mengine hapa nchini.
Amesema juhudi hizo zinajumuisha uchunguzi wa mapema wa ugonjwa, upatikanaji wa dawa muhimu, huduma za uchunguzi, kuimarisha uwezo wa wataalamu wa afya, kutoa elimu kwa jamii pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa damu salama na bidhaa za damu.
Vilevile, amesisitiza ushirikiano baina ya Tanzania na Terumo BCT utazidi kuimarishwa ili uweze kukuza tafiti, mafunzo kwa wataalamu wa afya, kuongeza uelewa wa jamii na kutumia teknolojia za kisasa katika uchakataji wa damu na matibabu ili kuboresha usalama na ubora wa huduma.
Amehimiza kampuni hiyo kushirikiana kwa karibu na wataalamu wa Wizara ya Afya ili kuhakikisha maeneo yote yaliyokubaliwa yanatekelezwa kwa vitendo na kuleta matokeo yanayopimika na kunufaisha Wananchi.