KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA JUHUDI ZA RAIS SAMIA KUFIKIA MALENGO YA 3 ZERO
Posted on: November 8th, 2026Na Shaban Juma, WAF – Kigoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha huduma za afya nchini kupitia malengo ya *3 Zero* yanayolenga kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na mtoto, kumaliza tabia ya wanawake kujifungulia nyumbani na kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa chanjo.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Emanuel Nuwasi, wakati wa ziara ya mafunzo kuhusu huduma ya mwambata wakati wa uchungu na kujifungua iliyofanyika katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Ujiji, mkoani Kigoma, Novemba 8, 2026.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema huduma ya mwambata wakati wa uchungu na kujifungua ni miongoni mwa afua zinazochangia kufikiwa kwa malengo ya *3 Zero*, kwa kumpa mama msaada wa karibu, faraja na kujiamini wakati wa uchungu na kujifungua.
Amesema huduma hiyo pia inahamasisha wanawake kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya kutokana na uwepo wa mazingira yanayozingatia usiri, staha, heshima na mahitaji ya mama, sambamba na maboresho ya miundombinu na utoaji wa huduma bora za uzazi.
Aidha, amesema huduma hiyo inaendana na falsafa ya Shirika lisilo la kiserikali la THAMINI UHAI, kwa kuwa inalenga kulinda maisha ya mama na mtoto, kuimarisha usalama wakati wa kujifungua na kuhakikisha wanawake wanapata huduma za uzazi zenye utu na heshima.
Aidha, wajumbe wa Kamati wamepata fursa ya kujionea utekelezaji wa huduma hiyo, kubadilishana uzoefu na wataalamu wa afya pamoja na kusikiliza maoni ya akinamama walionufaika na huduma ya mwambata wakati wa uchungu na kujifungua.