Wizara Ya Afya

TANZANIA ,PFIZER KUIMARISHA UPATIKANAJI WA DAWA NA HUDUMA BORA ZA AFYA NCHINI

Posted on: November 6th, 2026

Na Aisha Swahibu, WAF – Dar es Salaam

Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Bruno Sunguya, amesema ushirikiano kati ya Serikali kupitia Wizara ya Afya na Kampuni ya Dawa ya Marekani I Pfizer ni fursa muhimu ya kuimarisha upatikanaji endelevu wa dawa, chanjo na bidhaa za afya bora kwa gharama nafuu nchini.

Akizungumza Leo Novemba 6,2926 Jijini Dar es salaam wakati wa kufunga warsha ya uzinduzi wa ushirikiano wa makubaliano ya Tanzania kwa ajili ya Dunia yenye Afya Bora,Mganga Mkuu wa. Serikali Prof. Bruno Sunguya amesema ushirikiano huo unalenga kuunga mkono vipaumbele vya Serikali na kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za afya nchini.

Amesema ongezeko la idadi ya watu nchini linaendelea kuongeza mahitaji ya huduma za afya, hivyo ni muhimu kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya vina upatikanaji wa uhakika wa dawa na bidhaa tiba pamoja na kutoa huduma zenye ubora.

Prof. Sunguya ameeleza kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana kupitia ujenzi wa maelfu ya vituo vya kutolea huduma za afya na kusogeza huduma karibu na wananchi, bado kuna umuhimu wa kuimarisha upatikanaji wa dawa, hususan za magonjwa yasiyoambukiza kama saratani, magonjwa ya moyo na mishipa ya damu pamoja na magonjwa ya mfumo wa fahamu.

Prof. Sunguya amesisitiza umuhimu wa kupitia wigo wa dawa na bidhaa za afya zitakazojumuishwa katika ushirikiano huo ili kuongeza makundi yatakayokidhi mahitaji halisi ya wananchi, akipendekeza pia kuimarishwa kwa uratibu kupitia Kikosi Kazi cha Kitaifa kitakachoongozwa na Wizara ya Afya.

Aidha, ameeleza kuwa utekelezaji wa ushirikiano huo utatumia mifumo iliyopo ya Serikali badala ya kuanzisha mifumo sambamba, huku Bohari ya Dawa (MSD) ikiendelea kuwa chombo muhimu katika uratibu wa ununuzi na usambazaji wa dawa na bidhaa za afya.

Prof. Sunguya ameongeza kuwa ushirikiano huo unatoa fursa ya kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani na kuimarisha mifumo ya ugavi, akisisitiza kuwa ujuzi na uwezo utakaopatikana utaendelea kuwa rasilimali muhimu kwa nchi hata baada ya kipindi cha makubaliano kumalizika.