Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA, WHO WAIMARISHA UTAYARI WATUMISHI WA AFYA NYASA KUKABILIANA NA EBOLA

Posted on: November 3rd, 2026

Na Happyness Hans, WAF - Ruvuma

Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa ambaye ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Nyasa, Dkt. Hussein Ngaila, amesema ujio wa timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) umekuwa na manufaa makubwa kwa watumishi wa hospitali hiyo, hususan katika kuongeza uelewa na uwezo wa kujikinga na kuzuia maambukizi ya magonjwa ya milipuko, ikiwemo Ebola.

Akizungumza leo Novemba 3, 2026, Mkoani Ruvuma, Dkt. Ngaila amesema wataalamu hao wamefanya tathmini ya utayari wa hospitali hiyo kukabiliana na Ebola, ikiwemo kukagua maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya kuhudumia watu wanaoshukiwa kuwa na maambukizi, hata hivyo ameahidi kuyafanyia kazi mapungufu yote yaliyojitokeza ili kuboresha zaidi mifumo ya usalama hospitalini.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa magonjwa ya dharura na Maafa kutoka Wizara ya, Dkt. Fredirick Myula, amesema timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na WHO imeweka kambi katika Hospitali ya Wilaya ya Nyasa kwa lengo la kutathmini utayari wa hospitali hiyo na kuwajengea uwezo watumishi wa afya katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko, hususan Ebola.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha nchi inakuwa salama wakati wote, pamoja na kuwalinda watumishi wa afya dhidi ya maambukizi wanapokuwa wanapotoa huduma kwa wagonjwa wa magonjwa ya milipuko.

Naye Muuguzi Kiongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa amesema wamepata manufaa kutokana na maelekezo ya wataalamu hao kuhusu taratibu sahihi za kujikinga na magonjwa ya milipuko na kuzuia maambukizi endapo yatatokea katika maeneo mbalimbali nchini.