Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA, TAMISEMI ZATOA WITO WA KUHARAKISHA UWEKAJI WA MIKATABA YA CHW KIDIGITALI

Posted on: November 5th, 2026

Na Atley Kuni, WAF-Dodoma

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI zimewataka waratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma kwenye Halmashauri, kuhakikisha mikataba na nyaraka nyingine muhimu zinakamilishwa na kuingizwa katika mifumo ya kidijitali ili kuwezesha upatikanaji wa fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW).

Wito huo umetolewa Novemba 5, 2026 na Dkt. May Alexander Mratibu wa Huduma za Afya ngazi ya Jamii Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI, wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma wanao wasimamia Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii kutoka kwenye mikoa 12 na Halmashauri 25 zinazotekeleza mpango husika.

Katika mafunzo hayo, waratibu wameelezwa kuwa kukamilika kwa nyaraka zinazohitajika, zikiwemo mikataba, uthibitisho wa utekelezaji wa kazi (Proof of Work) na nyaraka za malipo (Payroll Documents), ni muhimu ili kuwezesha utoaji wa fedha zilizotengwa kwa mwaka wa fedha kupitia Mfuko wa Dunia wa kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu (TB) na Malaria (Global Fund).

"Mnatakiwa kushirikiana na viongozi wenu wa Halmashauri kuhakikisha nyaraka hizo zinakamilishwa kwa wakati, ili kuepusha ucheleweshaji wa fedha ambapo zisipotumika ndani ya muda uliopangwa zinaweza kurejeshwa na kuelekezwa katika maeneo mengine, ambayo yanauhitaji na inaweza isiwe hata nchini kwetu, kwa kuwa Mfuko.huo.hushughulikia nchi nyingi", amesema Alexander

Mafunzo hayo yanalenga kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali kwa usimamizi wa mikataba ya CHW, kurahisisha upatikanaji wa stahiki zao na kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Wizara ya Afya na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI zinaendesha mafunzo ya siku mbili kwa wataalam hao huku msisitizo ukowa kuendelea kusisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika kuboresha mifumo ya utoaji huduma na usimamizi wa rasilimali watu na fedha katika sekta ya afya.