WIZARA YA AFYA KUENDELEA KUIMARISHA UTEKELEZAJI MPANGO JUMUISHI WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII (CHW)
Posted on: November 4th, 2026Na Atley Kuni, WAF- Dodoma
Wizara ya Afya imesisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kutekeleza Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (iCCHW), huku ikiziomba Wizara, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, mikoa na Halmashauri kuimarisha ushirikiano na uratibu ili kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa ufanisi katika ngazi zote za utoaji huduma za afya nchini.
Hayo yameelezwa Novemba 4, 2026, na Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Dr. Rahma Hingora wakati akitoa neno la ufunguzi wa Kikao Kazi cha Viongozi na Waratibu wa Wizara ya Afya, OWM-TAMISEMI, Mikoa na Halmashauri kuhusu utekelezaji wa mpango huo, kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mtumba.
"Utekelezaji wa mpango huo ni dhamira ya kudumu ya Serikali na hakuna kurudi nyuma katika juhudi za kuunganisha programu mbalimbali za wahudumu wa afya ngazi ya jamii na kuwa mfumo mmoja jumuishi unaoratibiwa na kumilikiwa na Serikali", amesema Dkt. Hingora.
Hingora Amesema kuwa, katika awamu ya kwanza ya mpango huo umeanza kutekelezwa katika halmashauri 25 katika mikoa 12, ambapo Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHWs) wamepatiwa mafunzo, kusajiliwa na kupewa mikataba ya kazi.
Katika maelekezo yake, Hingora, amezitaka Taasisi na Mamlaka zinazohusika kujifunza kutokana na changamoto zilizojitokeza katika awamu ya kwanza, ikiwemo ucheleweshaji wa mikataba, malipo ya wahudumu, mapungufu ya nyaraka na kuchelewa kuanza kwa matumizi ya mfumo wa UCS.
Amesema kuwa, changamoto hizo zinapaswa kuchukuliwa kama fursa ya kuboresha utekelezaji, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha matumizi ya mikataba ya kidigitali na kuongeza umiliki wa mikoa na halmashauri kwa usimamizi wa malipo ya wahudumu hao.
Kikao hicho kinalenga kupitia hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mpango na uendelevu wake, kuwajengea uelewa viongozi kuhusu mfumo wa malipo na mikataba ya kidigitali ya CHWs, kupokea taarifa za utekelezaji kutoka mikoa 12 inayotekeleza mpango huo, pamoja na kukubaliana hatua za kuboresha utekelezaji kabla ya kuupanua katika halmashauri 159 zilizosalia kote nchini