Wizara Ya Afya

WAZIRI MCHENGERWA AWATAKA WANANCHI KUPIMA AFYA MARA KWA MARA

Posted on: August 23rd, 2026

Na Cletus Sanga, WAF – Kibiti

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kubaini mapema magonjwa na kupata matibabu kabla hali haijawa mbaya.

Akizungumza leo tarehe 23 Agosti 2026 wakati wa hafla ya kukabidhi ambulance Wilayani Kibiti, Mkoa wa Pwani, amesema Serikali haitaki kusubiri wananchi waumwe ndipo wawafikishe hospitalini, bali inahimiza kinga, uchunguzi wa mapema na matibabu kwa wakati.

Amesema magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya moyo, figo, kiharusi, saratani na magonjwa sugu ya mfumo wa upumuaji yanaongezeka, huku baadhi yake yakianza bila dalili zinazoonekana.

Mhe. Mchengerwa ametoa wito kwa wananchi kuzingatia kaulimbiu ya “JUA NAMBA ZAKO” kwa kupima shinikizo la damu, sukari, uzito na uwiano wake na urefu pamoja na kiwango cha mafuta mwilini, huku akiwataka kufuata ushauri wa wataalamu wa afya na kutumia dawa kwa usahihi.

Amesema wananchi wanapaswa pia kujikinga na magonjwa kwa kufanya mazoezi, kula mlo kamili wenye mboga na matunda, kupunguza chumvi, sukari na mafuta mengi, kuepuka tumbaku na matumizi mabaya ya pombe pamoja na kuweka mazingira safi na kufuata maelekezo ya wataalamu.

Aidha, amewataka wananchi kuripoti mapema dalili zisizo za kawaida au ongezeko la wagonjwa katika familia na jamii, huku Serikali ikiendelea kutekeleza mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuwawezesha Watanzania kupata huduma za afya kwa wakati bila kikwazo cha gharama.