Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA YAADHIMISHA SIKU YA USALAMA WA MGONJWA DUNIANI 2026

Posted on: September 17th, 2026

Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Usalama wa Mgonjwa Duniani 2026. Maadhimisho hayo yamefanyika kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kupitia mkutano wa mtandao wa Zoom. Maadhimizo yamelenga kuongeza uelewa kuhusu usalama wa mgonjwa na kuboresha huduma za afya, hasa kwa wagonjwa wenye magonjwa yasiyoambukiza.

Mwaka huu, maadhimisho hayo yamebeba mada isemayo “Huduma Salama kwa Magonjwa Yasiyoambukiza” na kaulimbiu “Huduma Salama kwa Maisha Yote.” Ujumbe huo unasisitiza umuhimu wa huduma salama na endelevu kwa wagonjwa katika hatua zote za maisha.

Akizungumza leo, Septemba 17, 2026, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Wizara ya Afya, Dkt. Hamad Nyembea, amesema utafiti na uelewa kuhusu usalama wa mgonjwa unaendelea kuongezeka hali hiyo inasaidia kuongeza mwamko kwa wananchi na watumishi wa afya pia inatoa nafasi ya kutambua mafanikio na kujifunza kutokana na changamoto zilizopo.

Dkt. Nyembea amesema usalama wa mgonjwa unahusisha kila hatua ya huduma. Unaanzia katika kumtambua mgonjwa kwa usahihi, kufanya uchunguzi na kumpatia matibabu sahihi pia ni kuhakikisha huduma zinapatikana kwa wakati na kusogezwa karibu na wananchi, kwa wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza, ufuatiliaji wa muda mrefu ni muhimu.

Amesema kila mgonjwa anapaswa kuhudumiwa kwa kuzingatia utu, haki na usalama wake. Ameongeza kuwa changamoto katika utoaji wa huduma zinaweza kuongeza madhara kwa mgonjwa, pia zinaweza kuongeza gharama kwa familia kutokana na vipimo au matibabu ya ziada.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kusogeza huduma za afya karibu na wananchi. Inaendelea pia kuboresha upatikanaji wa taarifa za afya.

Dkt. Nyembea amewataka wananchi kuepuka matumizi ya dawa bila ushauri wa wataalamu wa afya. Amesema matumizi sahihi ya dawa husaidia kuzuia madhara na kuokoa maisha.

Amesema maadhimisho hayo hayapaswi kuishia katika tukio la siku moja bali yawe chachu ya kuongeza uwajibikaji katika utoaji wa huduma za afya, kila mhudumu wa afya na mdau ana wajibu wa kuhakikisha huduma zinazingatia viwango vya usalama na utu w