Wizara Ya Afya

DKT. SAMIZI: TAKWIMU SAHIHI SILAHA YA KUTOKOMEZA MALARIA SADC

Posted on: September 22nd, 2026

Na Shaban Juma, WAF – Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence George Samizi, ametoa wito kwa nchi wanachama wa SADC kuimarisha ubora wa takwimu za malaria ili zitumike katika kupanga afua, kutenga rasilimali na kuongeza kasi ya kufikia lengo la kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030.

Dkt. Samizi ametoa wito huo leo Septemba 22, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akimwakilisha Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, katika ufunguzi wa Mkutano wa Kikanda wa Uthibitishaji wa Taarifa ya Mwaka ya Malaria ya SADC kwa mwaka 2026.

Amesema Tanzania, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa malaria na matumizi ya takwimu katika kufanya maamuzi, akisisitiza kuwa ubora wa takwimu ni msingi wa mafanikio katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

“Ubora wa mwitikio wetu dhidi ya malaria unategemea ubora wa takwimu zinazoongoza maamuzi yetu. Takwimu bora ndio msingi wa kulenga afua, kutenga rasilimali, kupima matokeo na kubaini changamoto zinazojitokeza,” amesema Dkt. Samizi.

Amesema takwimu sahihi na zinazopatikana kwa wakati zinawezesha nchi kubaini maeneo ambayo malaria inaongezeka au kupungua, makundi yanayoendelea kuathirika na iwapo afua zinazotolewa zinawafikia wananchi wanaozihitaji.

Aidha, Dkt. Samizi amesema mabadiliko ya mwenendo wa malaria, usugu wa dawa na viuatilifu, mabadiliko ya tabianchi pamoja na uhamaji wa watu yanaweza kuathiri maambukizi, hivyo mifumo imara ya ufuatiliaji ni muhimu katika kubaini mabadiliko hayo mapema na kuchukua hatua.

Amewataka washiriki wa mkutano huo kwenda zaidi ya kuthibitisha takwimu na kuchambua sababu za mafanikio, maeneo yenye changamoto pamoja na kukubaliana hatua za kuziba mapengo katika ukusanyaji, utoaji na matumizi ya taarifa za malaria.

Amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa SADC, Sekretarieti ya SADC na wadau wa maendeleo katika kuimarisha ufuatiliaji na matumizi ya takwimu ili kuharakisha juhudi za kutokomeza malaria na kufikia SADC isiyo na malaria ifikapo mwaka 2030.