RUKWA YAIMARISHA UWEZO WA TIMU ZA KUKABILIANA NA DHARURA ZA AFYA
Posted on: September 22nd, 2026Na Cletus Sanga, WAF – Rukwa
Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) imeendesha mafunzo ya Timu za Kukabiliana na Dharura za Afya (Rapid Response Teams – RRT) Mkoani Rukwa, yenye lengo la kuimarisha uwezo wa wataalamu wa afya katika kutambua, kuchunguza na kuchukua hatua za haraka dhidi ya milipuko ya magonjwa na dharura nyingine za afya ya jamii.
Akizungumza leo tarehe 22 Septemba, 2026 wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dkt. Ibrahim Mwita, amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuimarisha utayari wa Mkoa wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa na matukio mengine ya dharura za afya ya jamii, hasa kwa kuwa yanawaongezea wataalamu uwezo wa kufanya uchunguzi na kutoa mwitikio kwa wakati.
Dkt. Mwita amesema kuwa timu za mwitikio wa haraka zina nafasi kubwa katika kuhakikisha matukio ya afya yanatambuliwa mapema, taarifa zinawasilishwa kwa wakati na hatua stahiki zinachukuliwa kabla ya hali hiyo kuenea na kuleta madhara zaidi kwa jamii.
“Tunapaswa kuwa na timu zenye uwezo na utayari wa kukabiliana na matukio ya dharura wakati wowote yanapotokea, kwa sababu hatua za mapema na mwitikio wa haraka ni muhimu katika kulinda afya za wananchi,” amesema Dkt. Mwita.
Aidha, Dkt. Mwita amesema Mkoa utaendelea kuimarisha ushirikiano na wataalamu pamoja na wadau wa afya katika kujenga uwezo wa timu hizo, huku akisisitiza umuhimu wa uratibu, mawasiliano na matumizi sahihi ya taarifa katika kufanya maamuzi wakati wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa na dharura nyingine za afya.
Kwa upande wake, Afisa Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Mlipuko kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Boniface Makelemo amesema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uwezo wa wataalamu katika ufuatiliaji na mwitikio wa magonjwa ya mlipuko, pamoja na kuhakikisha timu za mwitikio wa haraka zina uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi wakati wa matukio ya dharura za afya ya jamii.