Wizara Ya Afya

BILIONI 5 KUKAMILISHA MIRADI HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA CHATO

Posted on: September 21st, 2026

Na Shaban Juma, WAF – Chato

Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga Shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato, ikiwemo jengo la kuhifadhia maiti, jengo la kufulia (laundry), jengo la damu salama pamoja na jengo la wodi.

Hayo yamesemwa leo Septemba 21, 2026 na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi na utoaji wa huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato, Wilaya ya Chato mkoani Geita.

Dkt. Samizi amesema Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwekeza katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya hospitali hiyo ili kuimarisha utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi, huku hospitali hiyo ikiwa tayari inatoa huduma za kibingwa na bobezi 15.

Amesema awamu ya kwanza ya ujenzi wa hospitali hiyo imegharimu Shilingi bilioni 13, ambapo fedha hizo zimetumika kujenga jengo la wagonjwa wa nje (OPD), famasi na maabara, jengo la huduma za dharura pamoja na Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU).

Aidha, amesema awamu ya pili ya ujenzi wa hospitali hiyo inagharimu Shilingi bilioni 18, huku Serikali ikiwa imetenga Shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kukamilisha baadhi ya majengo na miundombinu muhimu ambayo bado haijakamilika.

Ameeleza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaimarisha zaidi mazingira ya utoaji wa huduma katika hospitali hiyo na kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi wanaofika kupata huduma.

Dkt. Samizi amesisitiza watumishi wa hospitali hiyo kuzingatia ubora wa huduma, uadilifu na nidhamu kazini, akieleza kuwa uwekezaji unaofanywa na Serikali unapaswa kwenda sambamba na uwajibikaji na huduma bora kwa wananchi.

Ametoa wito kwa watumishi kuhakikisha miundombinu, vifaa na rasilimali zinazowekezwa na Serikali zinatumika ipasavyo kwa lengo la kuendelea kuboresha huduma za afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki kwa wakati.