WAZIRI MCHENGERWA ASISITIZA MATUMIZI SAHIHI NA UTUNZAJI WA AMBULANCE
Posted on: August 23rd, 2026Na Cletus Sanga, WAF – Kibiti
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha magari ya wagonjwa yanatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa, yanatunzwa kwa wakati na kuwa tayari muda wote ili kuongeza ufanisi wa huduma za dharura na kuokoa maisha ya wananchi.
Akizungumza leo tarehe 23 Agosti, 2026, katika hafla ya makabidhiano ya gari la wagonjwa kwa Wilaya ya Kibiti, Mkoa wa Pwani, Mhe. Mchengerwa amesema uwepo wa ambulance pekee hautoshi, bali kinachopaswa kupewa kipaumbele ni kuhakikisha gari hilo linafanya kazi wakati wote, lina vifaa muhimu na linaendeshwa na wahudumu wenye ujuzi.
Amesema huduma za dharura zinahitaji utayari wa muda wote kwa kuwa kuchelewa kwa dakika chache kunaweza kuleta tofauti kubwa kati ya uhai na kifo. Kwa hiyo, ambulance hiyo inapaswa kuwa tayari kuwafikia wagonjwa na majeruhi kwa wakati, wakiwemo wajawazito wenye dharura, watoto, waathirika wa ajali na wagonjwa wenye hali zinazohitaji huduma za haraka.
Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa kila mgonjwa anayehitaji huduma ya dharura anastahili kuhudumiwa kwa misingi ya kitaalamu na bila ubaguzi, huku akiwataka wananchi kutoa taarifa endapo gari hilo litatumika kinyume na madhumuni yaliyokusudiwa au endapo kutakuwa na ucheleweshaji wa huduma.
Aidha, amewataka waendesha pikipiki kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, hususan matumizi ya helmeti, akisisitiza kuwa hatua hizo ni muhimu katika kupunguza ajali zinazoweza kuzuilika na kuokoa maisha pamoja na nguvu kazi ya taifa.
Amesema ushirikiano kati ya wananchi, watoa huduma za afya na Serikali ni muhimu katika kuhakikisha ambulance hiyo inatunzwa na kutumika kwa ufanisi, wagonjwa wanafikiwa kwa wakati na huduma za dharura zinatolewa kwa usalama, weledi na kwa kuzingatia utu wa mgonjwa.