WATUMISHI WA AFYA KASULU WAJENGEWA UWEZO, UTAYARI KUKABILIANA NA EBOLA
Posted on: August 23rd, 2026Na WAF – Kigoma
Wizara ya Afya kupitia Idara ya Dharura na Maafa, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI pamoja na CIHEB -Tanzania chini ya Mradi wa Usalama wa Afya Duniani, imeendelea kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya katika Hospitali ya Wilaya ya Kasulu – Nyamyusi, mkoani Kigoma, kwa lengo la kuimarisha utayari wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko, hususan Ebola.
Akizungumza leo, Agosti 23, 2026, Mratibu wa Magonjwa ya Dharura kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Erick Richard, amesema Serikali inaendelea kuimarisha maandalizi kwa kuhakikisha vituo vilivyotengwa kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa na wahisiwa wa Ebola vinawezeshwa kwa vifaa tiba na mahitaji muhimu yatakayosaidia kukabiliana na magonjwa ya milipuko endapo yatatokea.
“Mafunzo haya yamefanyika leo na yamewahusisha watumishi wa afya ambao wamejengewa uwezo kwa vitendo kuhusu namna sahihi ya kumpokea na kumhudumia mgonjwa au mhisiwa wa Ebola, pamoja na matumizi sahihi ya vifaa vya kujikinga. Mapungufu yaliyobainishwa katika zoezi hili yamechukuliwa na kufanyiwa maboresho ili kuimarisha zaidi utayari,” amesema Dkt. Erick Richard.
Aidha, Dkt. Erick amewataka wananchi wa Mkoa wa Kigoma kuendelea kuchukua tahadhari na kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya, huku akisisitiza umuhimu wa kutoa taarifa mapema pale mtu anapoonekana kuwa na dalili zinazoweza kuashiria Ebola au magonjwa mengine ya milipuko.
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka CIHEB-Tanzania, Bi. Nuru Ndaweka, amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuwawezesha watumishi wa afya kupitia mafunzo pamoja na vifaa vya kujikinga, akieleza kuwa CIHEB inalenga kufikia vituo tisa vilivyotengwa katika Halmashauri nane za Mkoa wa Kigoma.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kasulu, Dkt. Mahamudu Mitenda, amesema mafunzo hayo yataongeza ufanisi na utayari wa watumishi wa afya katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko, Amesema watumishi wamepata uelewa zaidi kuhusu maandalizi, matumizi na uvaaji sahihi wa mavazi ya kujikinga, huku akiomba mafunzo hayo yaendelee kutolewa mara kwa mara ili kuimarisha utayari na usalama wa afya.