USIMAMIZI MADHUBUTI WASISITIZWA KUFANIKISHA UTEKELEZAJI WA BIMA YA AFYA KWA WOTE
Posted on: November 5th, 2026Na Andrea Kadege, WAF-Dodoma
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na uwajibikaji wa pamoja wa taasisi na sekta zote zinazohusika katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo leo Novemba 5, 2026, wakati wa Kikao cha Menejimenti ya Wizara ya Afya, akieleza kuwa pamoja na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuwa na jukumu la msingi katika utekelezaji wa mpango huo, Wizara ina wajibu wa kusimamia na kufuatilia utekelezaji wake ili kuhakikisha huduma hiyo inatolewa kwa ufanisi.
Amesisitiza umuhimu wa kila taasisi na sekta kutekeleza majukumu yake kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa, akieleza kuwa mafanikio ya mpango huo yanahitaji ushiriki na mchango wa kila mmoja katika kuhakikisha utekelezaji unakwenda kwa mwelekeo uliokusudiwa.
Aidha, amewataka viongozi na watendaji wote kuhakikisha wanazingatia mambo muhimu katika utekelezaji wa mpango huo, ikiwemo kuendelea kutoa elimu, kufanya ufuatiliaji na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu Bima ya Afya kwa Wote.
Vilevile, ameelekeza matumizi ya viongozi wa mikoa na wilaya pamoja na vyombo vya habari kuendeleza uhamasishaji na utoaji wa elimu kwa wananchi, akisisitiza kuwa juhudi hizo zinapaswa kuendelea hata katika maeneo ambayo tayari yamefikiwa na kampeni za uelimishaji.
Amesisitiza kuwa Bima ya Afya kwa Wote ni zoezi la kitaifa na si jukumu la taasisi moja au mtu mmoja, hivyo mafanikio yake yanategemea ushiriki, ushirikiano na uwajibikaji wa kila sekta katika kuhakikisha wananchi wanapata uhakika wa huduma za afya.