SERIKALI KUKAMILISHA MFUMO WA KITAIFA WA HUDUMA ZA AMBULANCE
Posted on: August 23rd, 2026Na Cletus Sanga, WAF – Kibiti
Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo wa kitaifa wa huduma za ambulance utakaolenga kuratibu kwa ufanisi zaidi huduma za dharura na kuhakikisha wananchi wanaopata dharura wanapata msaada kwa wakati na kwa usalama.
Akizungumza leo Agosti 23 ,2026 katika hafla ya kukabidhi ambulance kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Mkoa wa Pwani, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, amesema mfumo huo utahusisha vituo vya kupokea na kuratibu huduma za ambulance pamoja na mifumo ya ufuatiliaji wa magari.
Amesema Serikali inapanga kuunganisha huduma hizo na namba ya dharura *115 bila malipo* ili kuwezesha wananchi kupata msaada wa dharura kwa urahisi na huduma kuratibiwa kulingana na mahitaji.
Mhe. Mchengerwa amesema Serikali itaendelea kuongeza magari ya wagonjwa kadri yanavyohitajika na kujenga uwezo wa wahudumu wa Afya ili kuhakikisha huduma zinazotolewa kupitia ambulance zinakuwa salama na zenye ufanisi.
Aidha, amesisitiza kuwa uwekezaji katika ambulance hautakuwa na matokeo yaliyokusudiwa iwapo magari yaliyopo hayatatunzwa, akieleza kuwa matengenezo, upatikanaji wa matairi, betri na vipuri ni sehemu muhimu ya kuhakikisha magari yanabaki tayari wakati wote ili kutoa huduma kwa wananchi.
Amesema mafanikio ya mfumo huo yatapimwa kwa idadi ya ambulance zilizo tayari kufanya kazi, wagonjwa wanaofikiwa kwa wakati na maisha yanayookolewa, badala ya kuangalia idadi ya magari yaliyokabidhiwa pekee.