Wizara Ya Afya

KYERWA YAIMARISHA UTAYARI WA KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MILIPUKO

Posted on: August 23rd, 2026

Na Happyness Hans, WAF - Kagera

Wizara ya Afya kupitia Idara ya Dharura na Maafa, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI pamoja na CIHEB - Tanzania chini ya Mradi wa Usalama wa Afya Duniani, imeendelea na zoezi la usimamizi shirikishi wa huduma za dharura, ajali na wagonjwa mahututi, lengo likiwa ni kuimarisha utayari wa watumishi wa afya katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko katika Hospitali ya Wilaya ya Kyerwa, mkoani Kagera.

Akizungumza leo, Agosti 23, 2026, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kyerwa, Dkt. Richard Sangu, amesema wamepata fursa ya kujifunza na kujengewa uwezo katika masuala mbalimbali ya kukabiliana na magonjwa ya milipuko, ikiwemo namna ya kumpokea mgonjwa mwenye maambukizi au anayeshukiwa kuwa na virusi vya Ebola.

Dkt. Sangu amesema wamejengewa uwezo wa kufanya uchunguzi wa awali kwa wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na maambukizi (screening), taratibu sahihi za kumtenga mgonjwa (isolation), pamoja na namna wagonjwa na wahudumu wa afya wanavyopaswa kupita katika maeneo maalum kuanzia hatua ya awali hadi mwisho wa huduma.

Amesema changamoto zilizobainika wakati wa zoezi hilo zimepokelewa na uongozi wa hospitali, na zile zilizo ndani ya uwezo wao zitashughulikiwa kwa wakati ili kuhakikisha hospitali inakuwa tayari kutoa huduma endapo itampokea mgonjwa anayeshukiwa kuwa na ugonjwa wa mlipuko.

Kwa upande wake, Daktari na Mratibu wa Huduma za Tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Kyerwa, Dkt. Alex Donat, amesema wanaishukuru timu hiyo kwa kuwajengea uwezo na kuimarisha utayari wao wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko, hususan kutokana na Wilaya hiyo kuwa mpakani mwa nchi jirani ambayo tayari imekumbwa na ugonjwa wa Ebola.

Dkt. Alex amesema wamefundishwa namna ya kuwachunguza wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na maambukizi, maandalizi yanayopaswa kufanywa katika ngazi ya Wilaya, matumizi sahihi ya vifaa vya dharura, ikiwemo mashine maalum za kusaidia upumuaji na mashine ya kushtua moyo, pamoja na namna sahihi ya kufanya utakasishaji na utunzaji wa taka za kitabibu.