Wizara Ya Afya

AFRIKA KUWA NA SAUTI MOJA MABADILIKO YA MFUMO WA AFYA DUNIANI

Posted on: August 23rd, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF – Addis Ababa

Tanzania imesisitiza umuhimu wa Afrika kuwa na sauti moja, uongozi madhubuti na uwakilishi wenye nguvu kwenye maamuzi ya afya duniani ili kuhakikisha maslahi na vipaumbele vya Bara hili vinapewa uzito wakati wa mchakato wa mageuzi ya Muundo wa Mfumo wa Afya Duniani (Global Health Architecture – GHA).

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Afya Mhe. Dkt. Florence Samizi leo Agosti 23, 2026 jijini Addis Ababa, Ethiopia, akimwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa katika Kikao cha 'African High-Level Ministerial Committee' kuelekea Mkutano wa 76 wa Kamati ya Kanda ya Afrika ya Shirika la Afya Duniani (WHO AFRO RC76).

"Tanzania kama nchi tunaunga mkono kikamilifu mchakato wa mageuzi ya GHA na kuipongeza Africa CDC kwa kuteuliwa kuwa Taasisi ya kikanda ya afya katika mchakato huo, hatua inayotoa fursa kwa Afrika kushiriki kikamilifu kuamua mwelekeo wa mfumo wa afya duniani," amesema Dkt. Samizi

Akizungumzia umuhimu wa mageuzi hayo kwa wananchi, Dkt. Samizi amesema, mfumo wa afya duniani unapaswa kuzingatia mahitaji halisi ya nchi, ikiwemo upatikanaji wa fedha, teknolojia na uwezo wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa.

"Dunia kwa sasa inakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa fedha za afya, mabadiliko ya kijiografia na kisiasa pamoja na majadiliano kuhusu mkataba wa Kimataifa wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa, upatikanaji wa vimelea na mgawanyo wa manufaa (PABS)," amesema Dkt. Samizi

Aidha, Dkt. Samizi amesema mfumo mpya wa afya duniani unapaswa kuwa na mgawanyo wa majukumu ulio wazi kati ya taasisi za kimataifa, kikanda na kitaifa, kupunguza urudiaji wa majukumu na kuhakikisha fedha zinaelekezwa kwenye vipaumbele vya nchi.

Kwa upande wa hatua zinazofuata, Dkt. Samizi amezihimiza nchi wanachama kushiriki kikamilifu katika mashauriano ya kila mwezi kuhusu mageuzi ya GHA, huku akipendekeza Afrika CDC na WHO AFRO ziwakutanishe Mawaziri wa Afya wa Afrika ifikapo Novemba 2026, baada ya kukamilika kwa rasimu ya kwanza ya ripoti ya "GHA Joint Task Force", ili kupitia mapendekezo na kutoa mwongozo wa kisiasa.