ZINGATIENI USALAMA WA MGONJWA NA WAHUDUMIENI KWA KANUNI NA MIONGOZO
Posted on: March 27th, 2024
Na: WAF, Shinyanga
Mganga Mkuu wa Serikali Prof Tumaini Nagu amewahimiza watumishi sekta ya afya kuzingatia na kuweka kipaumbele cha usalama wa mgonjwa katika utoaji wa huduma na kuwahudumia kwa moyo mmoja kwa kuzingatia kanuni na miongozo ya Sekta ya afya.
Prof. Nagu ameyasema hayo leo Machi 27, 2024 alipotembelea kituo cha Afya Lunguya, kilichopo Halmashauri ya Mji wa Kahama kwa ajili ya kuangalia huduma Mkoba za madaktari bingwa wa Mama Samia.
Aidha Prof. Nagu amesema jambo la usalama wa mgonjwa lipewe kipaumbele kwakua ndio jukumu na dhamana kubwa katika kuihudumia jamii na kuwapa huduma bora.
"Jambo la usalama wa mgonjwa lipewe kipaumbele, tutumie kanuni na miongozo ya sekta ya afya na mtoe huduma kwa moyo mkunjufu, huduma itoke ndan ya mioyo yetu na sio kusukumwa". Amesema Prof Nagu
Pia, Prof Nagu amewaasa watumishi hao kuzipenda kazi zao na kuzingatia huduma kwa mteja ili ni pamoja na kuyapenda maeneo yao ya kazi kwani taaluma hiyo sio ambayo kila mtu anaweza kuifanya
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya Lunguya Mathias leonard Msobi kwa niaba ya watumishi wa kituo hicho wamemuahidi Mganga Mkuu wa Serikali Prof Nagu kuwajibika ipasavyo katika kuboresha huduma za afya na kuomba serikali iendelee kuboresha miundombinu ya kituo hicho ili kiweze kuendelea kutoa huduma bora zaidi.