Customer Feedback Centre

Ministry of Health

"ZINGATIENI NJIA ZA KUJIKINGA NA UGONJWA WA POLIO" - NYERERE

Posted on: September 21st, 2023

NA WAF, RUKWA


Wananchi wamehimizwa kuzingatia kanuni za kujikinga na ugonjwa wa polio ili kuzuia maambukizi ya virusi vinavyosababisha ulemavu wa kudumu au kifo.


Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Charles Makongoro akimuwakilisha waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Chanjo ya polio iliyofanyika kitaifa mkoani Rukwa katika viwanja vya Shule ya Msingi Ndua.


“Wizara ya afya inawahimiza wananchi kuzingatia njia za kujikinga na polio ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya vyoo, kutoa taarifa kwa watoto waliopooza ghafla na kunywa maji safi na salama”. Amesema Makongoro.


Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Nyerere ametoa wito kwa wakuu wa mikoa ya Katavi, Mbeya, Kigoma, Songwe na Kagera kusimamia ipasavyo zoezi la chanjo kuwafikia watoto walengwa wa chanjo ili lengo la Serikli liweze kutimia.


Aidha, Mhe. Nyerere amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa watoa huduma ili wawapatie watoto chanjo dhidi ya kuwakinga na virusi vya ugonjwa wa Polio.


“Ninawasihi wananchi wote kutoa ushirikiano kwa timu za wachanjaji katika maeneo yote ili watoto wote chini ya miaka minane waweze kupata chanjo ya matone dhidi ya ugonjwa wa polio”. Amesema Mhe. Nyerere.


Kampeni ya chanjo ya polio imeanza Tarehe 21 mpaka 24 Septemba 2023 katika mikoa ya Rukwa, Katavi, Mbeya, Songwe, Kigoma na Kagera na kuwafikia watoto 3,250,598.