Customer Feedback Centre

Ministry of Health

ZAIDI YA WANANCHI 2500 WAFIKIWA NA HUDUMA ZA KIBINGWA NA UBINGWA BOBEZI MBEYA RRH

Posted on: May 9th, 2025

Kambi ya Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan Nyanda za Juu Kusini iliyodumu kwa siku tano, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, imehitimishwa leo Mei 9, 2025 huku watu zaidi ya 2500 wakiwa wamehudumiwa kupitia huduma Mkoba.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, Dkt. Abdallah Mmbaga akizungumza na Madaktari bingwa hao leo Mei 9, 2025 amewashukuru kwa kujitoa kwao kuwahudumia wananchi pamoja na kuwajengea uwezo watumishi mbalimbali wa ngazi za chini katika utoaji huduma.

Dkt. Mmbaga amesema wastani wa watu zaidi ya 500 kila siku wamenufaika na huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika kambi hiyo ni upasuaji wa jumla, upasuaji wa mifupa, magonjwa ya wanawake na uzazi, magonjwa ya Ndani, sambamba na matibabu na upasuaji wa pua, koo na sikio,

Huduma nyingine za kibingwa zilizoolewa amesema ni za watoto, dawa za usingizi na ganzi, radiolojia, usikivu, macho, kinywa na meno, ipasuaji wa uso na taya.

Akizungumza kwa niaba ya madaktari bingwa Dkt. Msafiri Birigi, kutoka Hospitali ya Kanda Mbeya, amepongeza maandalizi yaliyofanyika na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, pamoja ushirikiano ambao watumishi wa hospitali hiyo wameonesha ikiwemo utayari wao katika kujengewa uwezo katika maeneo mbalimbali yao ya utaalamu.

Dkt. Mmbaga, ameahidi kuyafanyia kazi maoni yaliyopendekezwa na madaktari bingwa hao, sambamba na changamoto ya kukosekana kwa kipimo cha uchunguzi wa mfumo wa chakula (endoscopy)na kushauriana na uongozi wa hospitali kuchukua hatua muhimu za kuwezesha upatikanaji wa vipimo na uchunguzi katika eneo hilo.

Dkt. Gilbert Kwesi ambaye ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe, na Daktari Bingwa wa Upasuaji ameshauri kuimarishwa kwa mawasiliano miongoni mwa viongozi na watumishi wa hospitali hiyo ili kuendelea kuboresha utoaji huduma katika Hospitali hiyo.