Ministry of Health

WIZARA YAONGEZA UWEKEZAJI KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO

Posted on: August 12th, 2026

Na Shaban Juma, WAF - Dodoma


Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, amesema Serikali imeendelea kuongeza uwekezaji katika huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto kwa lengo la kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga nchini.


Dkt. Magembe ameyasema hayo leo, Agosti 11, 2026, jijini Dodoma, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kilichojadili taarifa kuhusu hali ya vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga pamoja na mikakati ya kukabiliana na vifo hivyo.


Amesema Serikali imeongeza uwezo wa vituo vinavyotoa huduma za dharura za uzazi na mtoto (CEmONC) kutoka vituo 566 hadi 627, hatua inayolenga kuhakikisha wanawake wanapata huduma muhimu kwa wakati wanapokabiliwa na changamoto wakati wa ujauzito, kujifungua na baada ya kujifungua.


Aidha, Dkt. Magembe amesema idadi ya wodi maalum za watoto wachanga (NCU) nchini imeongezeka kutoka 362 hadi 438 katika mwaka 2025/2026. Amesema Serikali pia inaendelea na ujenzi wa NCU 35 za kisasa katika Hospitali za Rufaa za Mikoa 15 na Halmashauri 20 ili kuongeza upatikanaji wa huduma bora kwa watoto wanaozaliwa wakiwa na changamoto za kiafya.


Amesema uwekezaji huo umeenda sambamba na kuongezeka kwa vifaa tiba muhimu kwa ajili ya huduma za watoto wachanga, ikiwemo mashine za CPAP ambazo zimeongezeka kutoka 130 mwaka 2025 hadi 1,780, pamoja na mashine za kutibu manjano, kutoa joto na kuzalisha oksijeni.


Dkt. Magembe amesema Serikali pia imeendelea kuongeza nguvu kazi katika sekta ya afya, ambapo jumla ya watumishi 53,633 wa kada mbalimbali wameajiriwa na kusambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini kati ya mwaka 2021 na Machi 2026.


Amesema Wizara itaendelea kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto kuanzia ngazi ya jamii hadi hospitali za rufaa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuhakikisha wanawake na watoto wanapata huduma salama na bora kwa wakati.


Amesema hatua hizo zinalenga kuchangia kufikiwa kwa azma ya Serikali ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi hadi chini ya vifo 70 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030.