Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WIZARA YA AFYA YAIKABIDHI ZIMAMOTO MAGARI YA UOKOAJI YENYE THAMANI YA BILIONI 1.6

Posted on: July 7th, 2023

Na. Catherine Sungura,Dar es salaam.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo Julai 8, 2023 amemkabidhi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Inj. Hamad Masauni Magari matatu ya uokoaji yenye zana za kisasa yenye thamani ya shilingi Bilioni 1.6 kwa ajili ya jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwenye hafla fupi iliyofanyika viwanja vya Zimamoto mkoa wa Ilala jijini Dar es salaam.

Waziri Ummy amesema magari hayo yamekuja wakati muafaka ambapo kwa sasa dunia inajiandaa kukabiliana na majanga, dharura na magonjwa ya milipuko hivyo magari hayo yataenda kutoa huduma za awali pindi ajali inapotokea ili kupunguza madhara yatokanayo na ajali au vifo.

Amesema Wizara yake ilianzisha mfumo rasmi wa huduma za dharura nje ya hospitali ikiwemo uokoaji wakati wa ajali ili kuwezesha majeruhi wa ajali kupata huduma ya kwanza eneo la tukio kabla ya kusafirishwa kwenye vituo vya kutolea huduma za tiba.

“Utolewaji wa Huduma za dharura nje ya hospitali (EMS) ni hatua muhimu utakaoweza kupunguza athari kwa majeruhi ikiwemo ulemavu pia gharama za matibabu kwa Serikali, mwananchi pamoja na vifo”.

Kwa upande wa takwimu kwa hapa nchini Waziri Ummy amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la majeruhi wa barabarani ambapo 47% ni majeruhi watokanao na ajali za pikipiki na jumla ya majeruhi wa ajali walioingia kwa dharura katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI) kwa mwaka 2021 walipokea majeruhi wa ajali 9,270 na mwaka 2022 walipokea majeruhi wa ajali barabarani 9,933.

Pamoja na hayo Waziri Ummy amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mara ya kwanza katika uongozi wake kuweza kujenga majengo ya dharura (EMD) hadi ngazi za wilaya yapatayo majengo 81 na hospitali za mikoa majengo 21 pia wodi za wagonjwa mahututi (ICU) 28 katika hospitali za wilaya na 45 katika hospitali za Mikoa, Kanda na Taifa.

Naye, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Inj. Hamad Masauni ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuwapatia magari hayo ambayo yanaenda kuongeza tija na kuondoa changamoto zilizokuwa zinaikabili jeshi hilo na kuahidi kuyatumia magari hayo ipasavyo.