Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WAZIRI UMMY MWALIMU ATOA WITO KWA WAZAZI NA WALEZI KUSIMAMIA KIKAMILIFU CHANJO KWA WATOTO

Posted on: December 27th, 2022

Na Englibert Kayombo, WAF - Dar Es Salaam.


Wito umetolewa kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wachanga wanapata chanjo zote muhimu zinazotolewa ili kuwajengea kinga imara ya kukabiliana na magonjwa.


Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alipokuwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke Jijini Dar Es Salaam ambapo amebaini kuna ongezeko la watoto wanaougua ugonjwa wa Surua.


“Nilitoa taarifa kwamba tunaona ongezeko la watoto wenye ugonjwa wa Surua nchini Tanzania na ongezeko hilo tunaliona katika WIlaya ya Temeke, Daktari ametuambia kuwa hapa wanapata watoto wanaougua ugonjwa wa Surua takribani watano kila siku katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke” amesema Waziri Ummy.


“Nitoe wito kwa Wazazi na Walezi wenzangu kuhakikisha kwamba watoto wao wanapata chanjo zote muhimu ikiwemo chanjo ya Kifua Kikuu, Polio, na Surua” amesisitiza Waziri Ummy Mwalimu


Waziri Ummy amesema kuwa Wizara ya Afya itaweka mpango jumuishi wa kuhakikisha kwamba wataalam wanapokwenda kutoa huduma za mkoba wajumuishe kutoa chanjo nyinginezo ikiwemo chanjo ya Surua.


“Tutahakikisha tunapokwenda nyumba kwa nyumba, Kijiji kwa Kijiji, Kata kwa Kata kutoa chanjo ya Polio tutoe pia chanjo ya Surua kwa sababu tumeona ongezeko ni kubwa sana la ugonjwa huu ambao unawezakuleta madhara makubwa sana na hata kupelekea kifo” amefafanua Waziri Ummy


Waziri Ummy amesema baadhi ya Wazazi na Walezi wamekuwa hawasimamiii vyema zoezi la chanjo kwa watoto na kusababisha watoto kukosa dozi kamili za chanjo hivyo kuwaweka watoto katika hatari ya kuugua.


“Watu wanachelewa, wanaona mtoto ameshafikisha miezi tisa anamuona haumwi ameshakuwa mkubwa hivyo wanapuuzia kusimamia ukamilishaji wa chanjo za mtoto” amesema Waziri Ummy Mwalimu huku akikemea hali hiyo na kuwataka Wazazi na Walezi kuwajibika kusimamia chanjo za watoto.


Aidha Amesema kuwa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Vyombo vya habari na Wadau wa Sekta wataendelea kutoa elimu ya umuhimu wa chanjo hizo kwa watoto ili Jamii iweze kufahamu na kuwa na uelewa mzuri zaidi juu ya manufaa ya chanjo.