WAZIRI UMMY AIPA MIEZI MIWILI TMDA KUFANYA UTAFITI WA SHISHA.
Posted on: May 31st, 2022
NA WAF - DOM
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ametoa miezi miezi miwili kwa TMDA kushirikiana na Tume ya madawa ya kulevya nchini kufanya utafiti wa shisha kuwekwa madawa ya kulevya.
Amebainisha hayo leo wakati akitoa tamko kwenye maadhimisho ya siku ya kutotumia tumbaku duniani yenye kauli mbiu isemayo "Tumbaku:tishio la mazingira yetu" kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma.
Amesema, "Maelekezo yangu ni kufanya tathimini ya bidhaa hizi ili kulinda afya za jamii kwani kufanya biashara ya shisha ujue unafanya kosa la jinai, Sheria ya kudhibiti matumizi ya bidhaa za tumbaku nchini sura ya 121 haijatekelezwa kikamilifu, TMDA mfanye tathimini kwa kina". Amesema Waziri Ummy.
Sambamba na hilo, Waziri Ummy amesema, Magonjwa mengi yasiyo ya kuambukiza yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku na kuleta maradhi mbalimbali yanayosababishwa na matumizi holela ya bidhaa za tumbaku.
"Jamii inatakiwa kupunguza au kuacha kabisa matumizi ya tumbaku au bidhaa zake kwa ajili afya zetu, kwani wanaotumia bidhaa ya tumbaku zaidi ya asilimia 50 wanafariki.
Aidha, Waziri Ummy amesema, takribani vifo 14,700 kwa mwaka hutokana na matumizi ya tumbaku na asilimia 8.7 ya watanzania sawa na watu milioni 2.6 hutumia tumbaku nchini.
Hata hivyo, amesema, uchunguzi unaonesha kuwa takribani asilimia 65 ya wavutaji hutupa vichungi vya sigara barabarani, kwenye fukwe za baharini na maziwa. Vilevile katileji nyingi za plastiki za sigara za kielektroniki huishia kutupwa kwenye mifereji ya maji na barabarani na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.
Pia, amesema watu wengi huathirika na moshi wa sigara katika maeneo ya kazi, kwenye baa, kumbi za starehe na migahawa ambapo utafiti ulionesha kuwa asilimia 77 ya watu huvutishwa sigara kwenye baa, asilimia 31.1 kwenye migahawa na asilimia 13.8 majumbani.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), utumiaji wa bidhaa za tumbaku husababisha vifo kwa karibu nusu ya watumiaji wake na zaidi ya watu takribani milioni 8 hufa kila mwaka duniani kwa sababu ya matumizi ya tumbaku.
Vilevile milioni 7 ya vifo hutokana na matumizi ya mojakwa moja,wakati milioni 1.2 ni kutokana na utumiaji wabidhaa za tumbaku usio wa moja kwa moja.