Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WAZIRI MHAGAMA, BALOZI POLEPOLE WAJADILI UZALISHAJI WA DAWA NCHINI

Posted on: May 3rd, 2025
Na WAF - Dodoma

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama leo Mei 03, 2025 amekutana na Balozi wa Tanzania nchini Cuba Mhe. Hamphrey Polepole lengo likiwa ni kujadili namna ya kushirikiana na nchi ya Cuba katika uzalishaji wa bidhaa za dawa pamoja na kubadilishana ujuzi ili kuboresha huduma za afya nchini.

Katika kikao hicho, Waziri Mhagama amesema uzalishaji wa dawa hizo utasaidia kuokoa maisha ya Watanzania wengi kwa kupunguza magonjwa yanayoambukiza ikiwemo Malaria pamoja na magonjwa yasiyoambukiza kama Figo pamoja na Saratani.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Cuba Mhe. Hamphrey Polepole amesema Wizara ya Afya iangalie namna ya kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano baina ya Tanzania na Cuba katika uzalishaji na upatikanaji wa bidhaa za dawa ikiwemo katika uzalishaji wa dawa za tiba asili.

"Ili kuboresha huduma zetu za afya tumejipanga kuhakikisha teknolojia, ujuzi na ubobezi wa uzalishaji wa dawa muhimu na dawa bunifu unapatikana Nchini kwa matumizi yetu na kwa ajili ya kuzihudumia nchi nyingine za Afrika." amesema Mhe. Polepole

Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe, Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe pamoja na Mfamasia Mkuu wa Serikali Bw. Daudi Msasi.