Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WAUGUZI WA AFYA WAPEWA ELIMU JUU UTOAJI WA HUDUMA KWA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA

Posted on: December 17th, 2022

Na. WAF - MWANZA

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Chama cha Kisukari Tanzania imetoa mafunzo kwa wauguzi 283 kutoka katika Mikoa mitano namna ya kuzuia, kudhibiti na kuwahudumia wagonjwa wa Magonjwa Yasiyoambukiza.

Haya ameyasema leo na Muuguzi Mkuu Mkoa wa Mwanza (RNO) Bi. Claudia Kaluli wakati akifunga mafunzo ya kuzuia na kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza kwa wauguzi kutoka katika vituo vya Afya vya Mikoa mitano.

"Ni matumaini yangu kwamba baada ya kupata mafunzo haya mtaenda kuongeza ufanisi katika kutoa elimu kwa wananchi wanaokuja kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya ili wachukue tahadhari na kuepuka vichocheo vya magonjwa yasiyoambukiza." Amesema Bi. Kaluli

Aidha Bi. Kaluli ameongeza kwa kusema kuwa, wananchi wataamini taarifa sahihi kutoka kwa wauguzi hao kuhusiana na kuishi mtindo wa maisha unaofaa ikiwemo kuacha tabia bwete na kufanya mazoezi, kuzingatia ulaji unaofaa, kuepuka matumizi ya pombe yaliyopita kiasi na kuepuka matumizi ya tumbaku.

Kwa upande wake Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza Bw. Shedrack Buswelu amewataka wauguzi hao kwenda kuimarisha tiba kwa kutoa tiba kwa wananchi pamoja na kuweka takwimu sahihi za wagonjwa katika vituo vya Afya.

"Kwa kuwa mmeshapata elimu hii sasa ni jukumu lenu kwenda kutoa tiba sahihi, kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wagonjwa na pia kama kuna tatizo kubwa tuwe wepesi wa kutoa rufaa." Amesema Bw. Buswelu

Nae, Mratibu wa Magonjwa Yasiyoambukiza, Ofisi ya Rais - TAMISEMI Bi. Jesca Mugabilo amesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo wauguzi hao wa kuandaa mpango kazi, kwenda kuboresha utoaji wa huduma kwa wagonjwa na kuibua wagonjwa wa Magonjwa Yasiyoambukiza.

Mafunzo hayo yamemaliza kwa Wauguzi wa vituo vya Afya vya Mikoa mitano ambayo ni Mwanza, Geita, Mara, Kagera na Simiyu ambapo wamejengewa uwezo katika kuzuia, kudhibiti na kutoa huduma kwa wagonjwa wa Magonjwa Yasioambukiza.