Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WATUMISHI SEKTA YA AFYA ZINGATIENI MAADILI YA KAZI ZENU

Posted on: May 9th, 2025

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amewataka watumishi wa sekta ya afya nchini kuzingatia maadili ya kazi zao na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

Dkt. Magembe ameyasema hayo Mei, 8 2025 jijini Arusha, wakati akizungumza na watumishi katika ziara yake ya kikazi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru.

Amesema kuwa kila mtumishi wa afya anatakiwa kufanya kazi kwa weledi, kuwa na mawasiliano mazuri baina yake, wagonjwa na ndugu wa wagonjwa, kutumia lugha nzuri yenye staha, kusilikiza kwa makini nini kilichomleta mgonjwa hospitali ili mwisho wa siku mgonjwa apatiwe matibabu stahiki na kupata nafuu au kupona kabisa.

"Wote hapa tumefundishwa namna ya kumuhudumia mgonjwa kuanzia kuchukua maelezo yake, kumpima hadi kumpa matibabu anayostahili kulingana na tatitzo lililomleta, unaporuka hatua yoyote lazima uishie kuleta madhara kwa mgonjwa"

“Niwakumbushe Mabaraza ya Kitaaluma yako kisheria na yanayo jukumu la kusimamia taaluma, maadili na weledi wa wana wataaluma na pia yanayo nguvu ya kuchukua hatua kwa mtaalamu yoyote. Ukishindwa kuzingatia maadili ya taaluma yako kulingana na kiapo ulichokula, hatutasita kukuchukulia hatua kulingana na sheria, kanuni na taratibu na inaweza hata kufikia hatua ya kufutiwa leseni au usajili wako na hivyo hutaweza kufanya kazi mahala popote, tusifike huko" amesisitiza Dr Magembe.

Aidha, Dr Magembe alisisitiza umuhimu wa wataalamu kuhudumia wagonjwa na kufanya kazi kama timu kwa sababu kila kada ni muhimu katika matibabu ya mgonjwa ili kuleta matokeo mazuri ya tiba zinazotolewa hospitalini.

Dkt. Magembe amewashukuru watumishi wote kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuwahudumia wananchi na kusisitiza umuhimu wa kufanya vizuri zaidi ili kutoa huduma bora kwa wananchi.