Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WATU ZAIDI YA ASILIMIA 97 WAPATIWA DAWA ZA KINGATIBA NCHINI

Posted on: January 30th, 2025

Na WAF – Dar es Salaam

Watu takribani laki 257,358 kati ya walengwa laki 265,217 sawa na asilimia 97 walipatiwa dawa za kingatiba za kutokomeza ugonjwa wa matende na mabusha kutoka kwenye Halmashauri za Mtama na Mtwara Mikindani kwa mwaka 2024 ili kuendelea kudhibiti na kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele nchini.

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Januari 30, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maadhimisho ya kilele cha siku ya magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Duniani yanayoenda sambamba na kauli mbiu isemayo “Tuungane, Tuchukue hatua, Tutokomeze Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele.”

Waziri Mhagama amesema kwa upande wa ugonjwa wa usubi, watu milioni 5,462,851 kati ya watu milioni 6,447,157 kutoka katika halmashauri 24 walipatiwa kingatiba ya ugonjwa huo ikiwa ni sawa na asilimia 85 kwa mwaka 2024.

“Watu milioni 1,603,425 kati ya watu milioni 1,967,143 kutoka halmashauri saba (7) za Ngorongoro DC, Monduli DC, Longido DC, Kiteto DC, Simanjiro DC, Mpwapwa DC na Kalambo DC, walipatiwa kingatiba za ugonjwa wa trakoma (sawa na asilimia 82), watoto wenye umri wa miaka mitano (5) hadi 14 wapatao milioni 9,896,694 walilengwa kupatiwa huduma ya kingatiba kwa ugonjwa wa minyoo ya tumbo ambapo hadi kufikia Desemba 2024 watoto 8,676,234 sawa na asilimia 88 walimeza kingatiba,” amefafanua Mhe. Mhagama.

Amesema upande wa ugonjwa wa kichocho walengwa wa kumeza kingatiba walikuwa watoto milioni 8,145,947 kati yao Watoto milioni 6,289,884 sawa na asilimia 77 walimeza kingatiba za ugonjwa huo ambapo walengwa hao walifikiwa katika halmashauri 171 sawa na asilimia 93 ya halmashauri zote.

Aidha, Waziri Mhagama amesema kuwa Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi Bilioni 38 katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024 kupitia mapato ya ndani, kwa lengo la kuendelea kutoa Huduma kwa wananchi za magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele zikiwemo utekelezaji wa juduma za upasuaji wa matende na mabusha, usawazishaji wa vikope pamoja na utoaji wa dawa za kingatiba kwa jamii.