WATOTO NCHINI KUNUFAIKA NA VYAKULA SALAMA, BORA NA VYENYE VIRUTUBISHO
Posted on: August 14th, 2026Na WAF - Morogoro.
Watoto nchini Tanzania wanatarajiwa kunufaika na juhudi za kuimarisha upatikanaji wa vyakula salama, bora na vyenye virutubishi muhimu, kupitia ushirikiano wa Serikali na wadau wa afya, lishe, viwanda, biashara na utafiti.
Juhudi hizo zimejadiliwa Agosti 12, 2026 Mkoani Morogoro kupitia Kikao cha Kamati ya Ushauri wa Kitaalamu ya First Foods Africa, kilichoandaliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara.
Kikao hicho kinalenga kuweka mikakati ya kuboresha upatikanaji, ubora na usalama wa vyakula vinavyofaa kwa watoto, pamoja na kuimarisha lishe katika hatua za awali za ukuaji.
Hatua hizo zinatarajiwa kusaidia kupunguza utapiamlo, udumavu na upungufu wa virutubishi, huku zikiwapa wazazi na walezi fursa pana ya kupata vyakula vya watoto vinavyokidhi viwango vya ubora.
Aidha, juhudi hizo zinafungua fursa kwa wazalishaji wa ndani kutumia malighafi zinazopatikana nchini kuzalisha vyakula bora vya watoto, jambo linaloweza kuchochea uzalishaji, ajira na biashara.
First Foods Africa Technical Advisory Committee huwakutanisha wataalamu kutoka sekta mbalimbali kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na kutumia ushahidi wa kisayansi katika kuimarisha lishe na mifumo ya chakula kwa watoto barani Afrika.
Ushirikiano huo unaweka msingi wa kuhakikisha watoto wanapata chakula salama na chenye virutubishi muhimu kwa ukuaji wa mwili na akili, huku Tanzania ikiimarisha uzalishaji wa ndani wa vyakula bora vya watoto.