WATOTO 400 WANUFAIKA NA MATIBABU KUPITIA CRDB MARATHON YA MSIMU WA TANO
Posted on: August 18th, 2024
Zaidi ya watoto 400 wamenufaika na matibabu ya magonjwa ya moyo kupitia michango ya CRDB Bank Marathon katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Hayo yamesemwa Leo Agosti 17, 2024 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, wakati wa hafla ya kukabidhi hundi ya shilingi milioni mia moja kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) katika msimu wa tano wa mbio hizo.
Dkt. Biteko amepongeza mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia mbio hizo, akisema zimekuwa na mchango mkubwa kwa jamii ya Watanzania. Ameeleza kuwa CRDB Bank Marathon imeendelea kuwa msaada mkubwa kwa watoto wanaohitaji matibabu ya moyo, na ameishukuru benki hiyo pamoja na wadau wote kwa juhudi zao za kuboresha afya ya wananchi.
"Mbio hizi zimeleta mafanikio makubwa kwa jamii, na leo tunaona matokeo yake kwa watoto zaidi ya 400 kupata matibabu kupitia msaada huu," amesema Dkt. Biteko.
CRDB Marathon imeendelea kuwa mfano bora wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma katika kuboresha huduma za afya nchini Tanzania.