Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WATOA HUDUMA ZA AFYA 600 WAJENGEWA UWEZO KUHUSU MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA NCHINI.

Posted on: December 15th, 2022

Na. WAF - Mwanza

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imewajengea uwezo Watoa huduma za Afya 600 kwa kuwapa mafunzo juu ya utoaji wa huduma za kuzuia na kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupambana dhidi ya magonjwa hayo.

Hayo yamebainishwa leo na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Thomas Rutachunzibwa wakati akifungua mafunzo ya Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza kwa watoa huduma za Afya nchini.

"Mafunzo haya yamekuja wakati muafaka ambapo Serikali ipo katika utekelezaji wa Mkakati Jumuishi wa III wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza 2021-2026 ili kuhakikisha watoa huduma wanaweza kutoa huduma bora nchini." Amesema Dkt. Rutachunzibwa

Ameendelea kusema kuwa, mafunzo hayo yanayoendelea kutolewa yanategemea kuwafikia watoa huduma za Afya msingi wapatao 3,000 kutoka Mikoa yote 26 hadi kufikia Desemba, 2023.

"Tayari kupitia mpango huu jumla ya Watoa huduma 577 wamekwishajengewa uwezo kutoka vituo vya Afya 138 katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Singida, Dar es Salaam, Pwani, Songwe, Lindi, Dodoma na Kigoma kwa awamu ya Kwanza, Pili, Tatu na Nne." Amesema.

Sambamba na hilo, ameweka wazi kuwa, mafunzo haya yanayofanyika sasa ni awamu ya tano ambapo hadi kufikia 16 Desemba 2022, jumla ya watoa huduma 630 kutoka katika vituo vya Afya vya mikoa mitano ambayo ni Mwanza, Geita, Mara, Kagera na Simiyu watajengewa uwezo wa kuzuia, kudhibiti na kutoa huduma bora za magonjwa yasioambukiza.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Chama cha Kisukari Tanzani (TDA) kwa lengo la kuwajengea uwezo watoa huduma za Afya Msingi ili waweze kutoa huduma bora kwa wagonjwa wa Magonjwa Yasiyoambukiza.