Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WATAKIWA KUKAMILISHA MAPEMA MKAKATI WA ELIMU YA AFYA KWA UMMA

Posted on: July 15th, 2025

Wajumbe wa Kikosi kazi kinachoandaa Mpango Mkakati wa Elimu ya Afya kwa Umma wametakiwa  

 kukamilisha mapema mchakato wa rasimu ya mpango mkakati huo 

 ili kutoa nafasi ya hatua nyingine muhimu za kuidhinishwa na kuanza kutekeleza.


Rai hiyo imetolewa  leo Julai 15, 2025 na Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma Dkt. Ona Machangu kupitia kikao kazi kinachofanyika jijini Dar es Salaam, akikiagiza kuongeza kasi ya utendaji na kukamilisha haraka ili hatua nyingine za kuhalalisha rasimu hiyo zifuate haraka iwezekanavyo.


Amesema, kuongezeka kwa wadau mbalimbali ni ishara ya wazi  ya  kazi nzuri inayofanywa na Wizara ya Afya kupitia Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, hivyo rasimu hiyo ikikamilika kwa haraka itaongeza  ubora na thamani ya mambo yanavyofanyika.


“Natamani baada ya kikao hiki  rasimu iende hatua zinazofuata, ni hatari kuendelea kutekeleza afua za elimu ya afya kama hauna  mikakati, sababu hili ni miongoni mwa mambo yaliyowekewa mkazo kwenye marejereo ya Mpango Mikakati ya Sekta ya Afya ni sera ambazo hazikamiliki,” ameeleza Dkt. Machangu.


Aidha, rasimu hiyo itakapokamilika italeta mapinduzi katika utoaji wa elimu ya afya kwa kutumia teknolojia ya kisasa na mifumo ya kidijitali kwa lengo la kuweka msingi wa kuboresha ubora, ufanisi, usambazaji, na upatikanaji wa huduma za elimu ya afya kwa jamii nchini.


Katika taarifa yake ya kikao kazi cha kuadhimisha rasimu ya mpango mkakati wa elimu ya afya kwa umma, Wizara inalenga kuhakikisha kuwa afua za elimu ya afya zinatolewa kwa kutumia ushahidi wa kisayansi, takwimu sahihi, na mbinu bora za kitaalamu.


Katika kuhakikisha utekelezaji wake, Wizara kupitia Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma imetengeneza zana za ukusanyaji na utoaji taarifa za afya ambazo ni sanifu na rahisi kutumia, Tafiti za ubunifu na utafiti shirikishi kwenye jamii zinatumika kuunda afua zinazojibu mahitaji ya kijamii na timu za elimu ya afya kupewa vifaa vya kidijitali, na programu za kudhibiti takwimu kwa ufanisi.