WATAALAM WA MAABARA WATAKIWA KUSIMAMIA WELEDI, MATUMIZI SAHIHI YA RASILIMALI
Posted on: September 10th, 2025
NA WAF – DAR ES SALAAM
Wataalam wa maabara nchini wametakiwa kusimamia kwa weledi eneo la kazi kwa kuhakikisha ubora wa huduma na matumizi sahihi ya rasilimali, ili kuboresha afya ya jamii na kuimarisha mifumo ya afya nchini.
Hayo yamesemwa na Makamu Mkuu wa Chuo MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa leo Septemba 10, 2025 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uongozi wa maabara duniani, Jijini Dar es Salaam.
Pro.Kamuhabwa amesema mpango huo utawasaidia wataalam wa Maabara za Afya kujengewa ujuzi wa kiuongozi na kuimarisha usimamizi wa huduma muhimu za afya.
Dkt. Kamuhabwa ameeleza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuimarisha uwezo wa viongozi wa maabara katika kujenga mahusiano kazini, kusimamia rasilimali, pamoja na kuandaa na kutekeleza mipango mikakati ya kuboresha huduma za maabara.
“Hii ni fursa muhimu kwa washiriki kupata maarifa ya kina ya kiuongozi na mbinu za kisasa za kuboresha huduma za maabara nchini,” amesema Dkt. Kamuhabwa.
Aidha, ameongeza kuwa mafunzo kwa vitendo yatawawezesha washiriki kutumia mbinu bora za kutatua changamoto zinazojitokeza katika sekta ya maabara na kuongeza tija katika utendaji wao wa kila siku.
Kwa upande wake, Mkuu wa huduma za Maabara kutoka Wizara ya Afya Bw. Reuben Mkala, amesema ubora wa huduma za maabara ni mhimili wa kuboresha huduma za afya kwa ujumla, hasa katika utambuzi wa magonjwa na kuhakikisha upatikanaji wa takwimu sahihi.
Amesisitiza kuwa mafunzo hayo ya uongozi yataongeza ufanisi wa wataalam wa maabara kwa kuwawezesha kusimamia mifumo ya huduma kwa weledi na kuzingatia viwango vya ubora vinavyotakiwa.