Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WANANCHI ZAIDI YA 500 WAJITOKEZA SIKU YA KWANZA KAMBI YA MADAKTARI BINGWA WA DKT. SAMIA MKOANI MBEYA

Posted on: May 6th, 2025

Na WAF - Mbeya

Wananchi zaidi ya 500 wamehudumiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya ndani ya siku ya kwanza tangu ufunguzi wa kambi hiyo hapo jana Mei 05, 2025.

Akitoa ripoti ya Mei 06, 2025, Mratibu wa Huduma za Kliniki, Mbeya RRH, Dkt. Ngwilo Mwakyusa amesema zaidi ya wananchi 500 wamejitokeza na kupatiwa huduma za afya ikiwepo ya upasuaji.

Wananchi hao wamenufaika na mpango wa Mhe. Rais Dkt. Samia unaolenga kusogeza huduma za kibingwa na ubingwa bobezi karibu na wananchi, pamoja na kuwajengea uwezo watumishi waliopo ngazi za utoaji huduma.

Katika Kambi ya Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi ambao wameweka kambi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya wanahudumia wananchi kwa ubingwa na ubingwa bobezi kwenye magonjwa ya moyo, magonjwa ya figo, upasuaji rekebishi,upasuaji wa ubongo, mfumo wa mkojo, magonjwa ya saratani, upasuaji wa macho, afya ya akili, upasuaji wa sikio, pua na koo, upasuaji wa mifupa, upasuaji wa jumla, upasuaji wa kinywa na meno, matibabu ya watoto, magonjwa ya wanawake na uzazi, huduma za tiba ya viungo na utengamao

Malengo mahususi ya Serikali kupitia Wizara ya Afya ni kuimarisha afya za wananchi na kuhakikisha kila Mtanzania anapata matibabu stahiki bila kikwazo cha kufuata huduma za kibingwa mbali na maeneo yao.