Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WANANCHI UYUI WATAKIWA KUITUMIA, KUITUNZA ZAHANATI

Posted on: December 21st, 2024

Na WAF - Uyui, Tabora

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amewataka wananchi wa kijiji cha Simbodamalu kilichopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Uyui Mkoani Tabora kuitumia zahanati ya kijiji hicho kwa kwenda kliniki pindi wakina mama wakiwa wajawazito pamoja na kuitunza ili iendelee kutoa huduma za afya.

Waziri Mhagama ametoa wito huo leo Desemba 21, 2024 wakati akizindua zahanati ya Simbodamalu pamoja na wodi ya mama na mtoto iliyopo katika kata ya Lutende ambayo itasaidia kutoa huduma za afya katika kijiji hicho.


"Wakina mama tumieni zahanati hii kwa kuja kupata huduma za kliniki mnapokuwa wajawazito ili tuendele kupunguza vifo kwa akina mama na watoto pamoja na magonjwa ya fistula kwa kuwa hii ni dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan," amesema Waziri Mhagama

Aidha, Waziri Mhagama wakati akiwa katika wodi ya mama na watoto iliyopo katika kata ya Lutende kijijini hapo, ameahidi kuchagia vitanda vinne vya kisasa vya kujifungulia wajawazito, magodoro, pamoja na mashuka ili huduma ziendelee kutolewa katika wodi hiyo.

Waziri Mhagama baada ya kukagua nyumba ya mganga katika Kituo cha Afya Lutende amewaomba tena wadau wa sekta ya afya ambao ni Shirika la Kimataifa la World Vision Tanzania kuongeza milioni 50 ili ujenzi ukamilike pindi inapotokea changamoto yoyote kwa muda wowote, daktari awepo karibu na eneo la kazi.

Zahanati hiyo ya Simbodamalu pamoja na wodi ya mama na mtoto iliyopo katika kata ya Lutende zimejengwa kwa ushirikiano wa Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wananchi pamoja na wadau wa sekta ya afya ambao ni World Vision-Tanzania.

Katika hatua nyingine Waziri Mhagama amewaahidi wananchi wa kijiji hicho kuwaletea gari la wagonjwa (Ambulance) ili kurahisisha huduma za dharura hasa za wakina mama wajawazito pindi zitakapohitajika kwakuwa dhamira ya Rais Dkt. Samia ni kuona afya za wananchi wake zina imarika.