Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WAMILIKI VITUO VYA OPTOMETRIA NCHINI WATAKIWA KUHUISHA TAARIFA ZAO KWENYE MFUMO

Posted on: August 17th, 2025

Na WAF, Mbeya

Msajili wa Baraza la Optometria nchini Bw. Sebastiano Millanzi amewataka wamiliki wa vituo vinavyotoa huduma za optometria kuhuisha taarifa zao kupitia mfumo ya kielectroniki wa Health Facilities Registration System (HFRS).

Bw. Millanzi ametoa wito huo Septemba 16, 2025 mkoani Mbeya wakati wa zoezi endelevu la Usimamizi Shirikishi kwenye vituo mbalimbali vya afya vinavyotoa huduma ya optometria.

“Tulikuwa na zoezi kama hili mikoa ya kanda ya ziwa na kaskazini, kubwa tunaloendelea kusisitiza ni kila mmoja wetu ambaye ameamua kutoa huduma hii lazima ahuishe taarifa za kituo katika mifumo rasmi ili atambulike,” amesema Bw. Millanzi.

Mbali na kuwataka wamiliki hao kuhuisha taarifa zao kwenye mfumo, amewataka wamiliki wote kutenga vyumba kulingana na mahitaji ya shughuli zinazotendeka za Optometria.

“Maabara ya Optometria haitakiwi kuingiliana na sehemu ya kumsikiliza mgonjwa; rai yangu kwenu, hili liwe zingatio kwa wote ambao wameamua kutoa huduma hizi,” amesema Bw. Millanzi.

Pia Bw. Millanzi amesema bado wapo baadhi ya watu wasio waaminifu ambao wamevamia kada hiyo na wakiona ukaguzi upo kanda hii wenyewe wanakimbilia kanda nyingine, sasa ili kukabiliana nao lazima timu za afya za mikoa na halmashauri zote nchini kuendelea na mazoezi kama haya.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Bw. Charles Kalidushi amesisitiza suala la uzingatiaji wa usafi mahala pa kazi.

Kikosi kazi hicho kinachoongozwa na Msajili wa Baraza la Optometria kimejumuisha wataalam kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, mkoa wa Mbeya pamoja na Wataalam wa Halmashauri.

Waratibu wa huduma za macho mkoa na Jiji wameonesha kufurahishwa na zoezi hilo, huku wakiliita kama darasa huru litakalokuwa endelevu katika kutekeleza majukumu yao.