WAHUDUMU WA AFYA WAPEWA MAFUNZO KUKABILIANA NA MAGONJWA YA YALIYOKUA HAYAPEWI KIPAUMBELE
Posted on: February 2nd, 2025
NA WAF - MTWARA
Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Kongwa Trachoma Project (KTP) imeendelea kupambana na magonjwa yaliyokua hayapewi kipaumbele kwa kuwapatia mafunzo wahudumu wa afya kuanzia ngazi ya msingi ili kuongeza uelewa wa namna bora ya kushughulikia magonjwa haya.
Hayo yamesemwa tarehe 31 Januari 2024 na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Nanyamba Abdallah Jamali Kapende wakati wa maadhimisho ya Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele mkoani Mtwara.
“Tuhamasishe umma kufahamu namna magonjwa haya yanavyoambukizwa, dalili zake, na jinsi ya kuyatibu, hususan kwa wale waliokwisha athirika,” amesema Bw. Abdallah.
Bw . Abdallah amesema Kambi hii imefanyika wilaya ya Nanyamba ikiwa ni sehemu ya kampeni inayolenga kutoa huduma katika wilaya sita za mkoa wa Mtwara. Kampeni hii inalenga kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa kuwapatia elimu, uchunguzi, na matibabu ya magonjwa haya ili kupunguza maambukizi.
Kwa upande mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Dkt. Benedicto Ngaiza ameishukuru serikali kwa kuendelea kuleta miradi inayogusa sekta ya afya na ameahidi kuwa watausimamia mradi huu kwa ukaribu ili kuhakikisha unatoa huduma bora kwa wananchi.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kinga Wizara ya Afya, Dkt. Otilio Flavian Gowelle, amesema Mkoa wa Mtwara umekuwa kinara katika utambuzi wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele. Hili limefanikiwa kwa kushirikisha wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambao hutembelea kila nyumba na kila kata kuwatambua wagonjwa mapema na kuwapeleka kwenye vituo vya afya kwa matibabu.
Dkt. Otilio amesisitiza kuwa magonjwa kama kichocho na minyoo yanayoathiri watoto yanahitaji juhudi za pamoja kuyadhibiti. Serikali imeweka mikakati ya kumezeshwa dawa kila mwaka kwa watoto ili kupunguza maambukizi. Amewataka wananchi kushirikiana na wataalamu wa afya wakati wa kampeni hizi kwa kuhakikisha watoto wanapatiwa dawa ipasavyo.