WAGONJWA 500 KUFANYIWA UPASUAJI WA MTOTO WA JICHO BURE CHUNYA
Posted on: November 21st, 2024NA WAF - MBEYA
Wagonjwa 500 wa Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya, na maeneo ya jirani wanatarajiwa kunufaika na kambi ya huduma mkoba ya matibabu ya kibingwa kwa kufanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho bila malipo katika kipindi cha siku saba.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhe. Mbarak Batenga, Novemba 20, 2024, alipokuwa akiwajulia hali wagonjwa wanaopatiwa matibabu ya macho katika kambi maalumu ya matibabu ya mtoto wa jicho inayofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya.
Mhe. Batenga ameishukuru Serikali kwa juhudi inazofanya kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi wa maeneo ya vijijini, hususan wale wenye mahitaji maalumu ya matibabu.
“Katika Wilaya ya Chunya kuna tatizo kubwa la ugonjwa wa mtoto wa jicho, hivyo zinapokuja fursa kama hizi za matibabu, tunazichangamkia kwa sababu zinatoa suluhisho la moja kwa moja kwa matatizo haya ya macho na kusaidia kuboresha afya ya jamii,” amesema Mhe. Batenga.
Ameongeza kuwa, awali wananchi walihitajika kusafiri hadi Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya ili kupata huduma hii, lakini kupitia kambi hiyo, huduma zinatolewa hapo Chunya bila gharama yoyote, jambo ambalo limeleta unafuu mkubwa kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Helen Keller, Dkt. George Kabona, amesema kuwa shirika hilo linaendelea kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika jitihada za kuboresha huduma za afya ya macho kwa wananchi wa maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya.
Naye Daktari Bingwa wa Macho na kiongozi wa timu ya wataalamu, Dkt. Barnabas Mshangila, amesema kuwa kambi hiyo inatoa fursa kwa wagonjwa wengi ambao hawana uwezo wa kugharamia matibabu ya mtoto wa jicho.
Kambi hii ya matibabu ni hatua muhimu ya kusaidia jamii ya Wilaya ya Chunya kupambana na changamoto ya mtoto wa jicho na kuboresha hali ya maisha ya wananchi kupitia huduma za afya bora.