WAFANYABIASHARA WAPATIWA ELIMU YA MPOX
Posted on: April 8th, 2025
Na WAF, Dodoma
Wafanyabiashara nchini wametakiwa kuzingatia elimu ya namna bora ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko hasa ugonjwa wa Mpox ili waweze kutekeleza majukumu yao yakujitafutia kipato.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma Dkt. Ona Machangu Aprili 7, 2025 Jijini Dodoma wakati wa zoezi la utoaji wa elimu ya afya na upimaji wa afya bure katika soko la ‘Machinga Complex’ ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Afya Kitaifa.
Dkt. Machangu amesema kundi la wafanyabiashara ni kundi muhimu kutokana na muingiliano wao na watu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, hivyo Serikali kupitia Wizara ya Afya inatambua umuhimu wa kundi hilo kupatiwa elimu hasa ya magonjwa ya mlipuko kama Mpox.
“Tunaendelea kutoa elimu ya ugonjwa wa Mpox kwa wananchi ili waendelee kuchukua tahadhari na kujikinga, mwananchi akiweza kuzingatia maelezo ya ugonjwa wa Mpox itasaidia kujikinga yeye na hata watu wanaomzunguka” amefafanua Dkt. Machangu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto Dkt. Leonard Subi amesema kuwa magonjwa ya kuambukiza hayana mpaka kutoka kwa binadamu na wanyama hivyo kusababisha maambukizi na hatimaye kifo hivyo ni vizuri wananchi kuendelea kupatiwa elimu juu ya magonjwa haya ya mlipuko.
“Tuko hapa Machinga Complex kwa lengo la kuwafikia wafanya biashara ikiwa ni kwa mara ya kwanza Taifa la Tanzania linaadhimisha wiki ya Afya, hivyo tunayafikia makundi mbalimbali na kuwapatia elimu ya Afya, kutoa huduma za upimaji wa afya na kujibu masuali yao,” ameeleza Dkt. Subi
Ameongeza kuwa maadhimisho ya Wiki ya Afya ni muhimu kwa Watanzania kwakuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imeweza kuwafikia Watanzania lakini pia kujitathmini juu ya hali ya utoaji wa huduma tulipotoka, tulipo na tunapokwenda ili kufikia lengo la kila Mtanzania kupata huduma bora za afya zilizo karibu naye.
Dkt. Gasper Kisenga, Kaimu Mganga Mkuu wa Dodoma jiji, ameishukuru Wizara ya afya kwa kufika eneo la Machinga Complex na kutoa elimu ya Afya kwa wananchi na wafanyabiashara wa eneo hilo na kutoa huduma za upimaji bure kwa wananchi.