WAANDISHI WA HABARI, WAANDAAJI WA MAUDHUI WAANDALIWA KUWA MABALOZI WA AFYA YA UZAZI KWA VIJANA KUPITIA JIONGEZE360.
Posted on: August 14th, 2026WAANDISHI WA HABARI, WAANDAAJI WA MAUDHUI WAANDALIWA KUWA MABALOZI WA AFYA YA UZAZI KWA VIJANA KUPITIA JIONGEZE360.
Na ABDU MADENGE, WAF - Dar es Salaam.
Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo imeandaa semina ya siku tatu kwa waandishi wa habari, wahariri na waandaaji wa maudhui ya mitandaoni kwa lengo la kuwajengea uwezo kuwa mabalozi wa afya ya uzazi kwa vijana kupitia Bonanza la Afya ya Uzazi kwa Vijana (ARH) – JIONGEZE360, lenye kaulimbiu isemayo “Maamuzi Yako, Kesho Yako.”
Semina hiyo inayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Agosti 12 hadi 14, 2026, inalenga kuwawezesha washiriki kupata uelewa wa kina kuhusu afya ya uzazi kwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 na kuwapa maarifa yatakayowawezesha kuandaa maudhui sahihi, yenye ushawishi chanya na yanayochochea vijana kufanya maamuzi bora kuhusu afya zao.
Kupitia mafunzo hayo, waandishi wa habari watapatiwa uelewa kuhusu afya ya uzazi kwa vijana, huduma rafiki zinazopatikana, namna ya kuhamasisha vijana kupima afya zao pamoja na mbinu za kuripoti masuala ya vijana kwa usahihi, weledi na uwajibikaji.
Aidha, watajengewa uwezo wa kukabiliana na taarifa potofu, imani zisizo sahihi, unyanyapaa na ubaguzi unaowazuia vijana kupata huduma muhimu za afya. Semina hiyo pia itatoa nafasi kwa washiriki kujadiliana na wataalamu wa afya kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana nchini, ikiwemo mimba za utotoni, maambukizi ya VVU na magonjwa ya ngono, ukatili wa kijinsia, afya ya akili, lishe pamoja na saratani ya shingo ya kizazi.
Wizara ya Afya inaamini vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuelimisha jamii na kuwasaidia vijana kupata taarifa sahihi zinazoweza kubadilisha maisha yao na inatarajia baada ya mafunzo hayo waandishi wa habari na waandaaji wa maudhui kuwa mabalozi wa JIONGEZE360 kwa kuandaa na kusambaza taarifa sahihi zinazotokana na ushahidi, kuhamasisha vijana kushiriki katika bonanza, kutangaza huduma zitakazotolewa pamoja na kuibua mijadala chanya kuhusu afya ya uzazi kwa vijana.
vyombo vya habari vikichukua nafasi ya mbele katika kuwafikia vijana kwa taarifa sahihi za afya, itasaidia kupunguza upotoshaji na kuchochea matumizi ya huduma rafiki kwa vijana.