VIWANDA VYA KUZALISHA VIFAA TIBA KUONGEZEKA NCHINI
Posted on: July 13th, 2025
Na WAF - Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imetia saini ya makubaliano na kampuni ya kuzalisha vifaa vya maabara Abbott ya nchini Marekani yenye lengo la kujenga kiwanda kipya nchini kitakachoongeza upatikanaji wa vifaa tiba vitakavyosaidia kutambua magonjwa mbalimbali kwenye vituo vya afya.
Akizungumza katika utiaji saini wa makubaliano hayo Julai 12, 2025 Jijini Dodoma, Waziri wa afya Mhe. Jenista Mhagama amesema, kuongeza uzalishaji wa bidhaa tiba ndani ya nchi ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ili kupunguza gharama za utegemezi wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.
Amesema, kuanzisha kiwanda cha uzalishaji wa vifaa tiba nchini kutafanya Tanzania kuwa kituo cha umahiri kwenye tiba, kupunguza utegemezi wa kuagiza nje kwa asilimia 20 na kurahisisha upimaji wa magonjwa kama Virusi Vya Ukimwi, Kaswende na homa ya Ini.
“Sasa tunapokwenda ni kuzuri zaidi na niliwaambia tuna vipaumbele 10, kimojawapo ni kuongeza uzalishaji wa bidhaa tiba ndani ya nchi na kupunguza utegemezi kutoka nje ya nchi, tunashukuru sana kwa uwekezaji uliofanywa tumeweza kupunguza utegemezi kutoka asilimia 100 mpaka asilimia 80,” amesema Waziri Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagama amesema dhima ya Serikali ya awamu ya sita ni kuwekeza fedha nyingi kwenye Wizara ya Afya kwa lengo la kuongeza huduma zenye tija kwa wananchi ikiwemo matumizi ya teknolojia na mifumo ya akili mnemba itakayorahisiha utolewaji wa tiba kwa wananchi.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Uendeshaji Kibiashara, Idara ya Magonjwa ya Kuambukiza kutoka kampuni ya Abbott, Bw. Steven Henn amesema makubaliano hayo yaliyoanza mwezi Oktoba 2024, yamekuja yakiwa na nia ya dhati ya kuboresha huduma za afya kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Abbott.
"Kupata nafasi hii ya kuweka rasmi makubaliano haya yatakayokuwa ya muhimu kati ya Abbot na Wizara ya Afya kutufikisha kwenye hatua kubwa ya uwajibikaji wenye lengo la kuboresha huduma za afya," amesema Bw. Henn.
Naye, Mfamasia Mkuu wa Serikali Bw. Daudi Msasi amesema makubaliano hayo yana nia ya kuleta mabadiliko ikiwemo kupunguza gharama zilizokuwa zikitumika na Serikali kuagiza vifaa tiba nje ya nchi vilivyogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 51 kila mwaka.
“Pesa hiyo tulitumia kuagiza bidhaa nchini kwa ajili ya upimaji wa UKIMWI, homa ya ini na homa ya kaswende kwakuwa ni vitu ambavyo tunavipima pamoja kwa ajili ya kuzuia maambukizi kuendelea kuongezeka kwa wananchi,” ameeleza Bw. Msasi.