Customer Feedback Centre

Ministry of Health

VITUO VYA OPTOMETRIA VISIVYOSAJILIWA VINASTAHILI KUFUNGIWA

Posted on: April 17th, 2025

Na WAF, KILIMANJARO 


Mganga Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Jerry Khanga ameipongeza Timu ya Usimamizi Shirikishi kutoka Baraza la Optometria nchini kwa hatua ya kuvifungia vituo bubu vilivyokutwa vikitoa huduma za optometria bila ya kusajiliwa pamoja na huduma hizo kutolewa na watu wasiokuwa na taaluma ya optometria.


Dkt. Khanga ametoa pongezi hizo muda mfupi mara baada ya kupokea Taarifa ya Usimamizi Shirikishi iliyowasilishwa kwake Aprili 16, 2025 na Msajili wa Baraza la Optometria nchini Bw. Sebastiano Millanzi. 


"Nimepokea taarifa kutoka Same kuwa mmevifungia vituo viwili ambavyo vilikuwa vikitoa huduma kinyemela bila kuwa na usajili pamoja na kukosa wataalam wenye sifa husika, kitendo ambacho ni hatari kwa afya ya macho ya wananchi pia ni kinyume na Sheria ya Optometria Sura 23 ya mwaka 2007 niwapongeze sana," amesema Dkt. Khanga.


Dkt. Khanga ameongeza kuwa lazima Sekta ya Afya iangaliwe kwa mapana yake kwani wamiliki wa vituo hivyo vya Same ni sehemu tu ya walio wengi ambao kwa makusudi wameamua kukiuka utaratibu na miongozo iliyowekwa na Serikali.


Awali akiwasilisha taarifa ya zoezi hilo kwa mkoa wa Kilimanjaro Msajili wa Baraza Bw. Sebastiano Millanzi amemuelezea Mganga Mkuu huyo kuwa mbali na kuvifungia vituo hivyo, pia wametoa elimu kwa wamiliki hao pamoja na kuwapa mwongozo wa kufuata ili vituo vyao viweze kusajiliwa.


"Wapo wamiliki ambao vituo vyao vimesajiliwa lakini mapungufu yapo kwa watoa huduma; hawa tumewapa elimu na muda wa ķuhakikisha wanatafuta wataalam wenye sifa na kuachana na vishoka," amesema Bw. Millanzi.


Naye Msimamizi wa huduma za Macho nchini kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Kalidushi Kubingwa ameendelea kuwahimiza wananchi kuhakikisha wanajiridhisha na maeneo wanayokwenda kupatiwa huduma za macho kwani katika siku za hivi karibuni vishoka wamekithiri.