VIJANA WAMETAKIWA KUJITAMBUA KWA KUPIMA UKIMWI
Posted on: December 1st, 2023
Na. WAF - Morogoro
Vijana wa kiume wametakiwa kujitambua na kuthamini maisha yao kwa kupima UKIMWI ili kujua hali zao na kujikinga na maambukizi mapya ya VVU kwa lengo la kuutokomeza ugonjwa huo ifikapo 2030.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ametoa wito huo leo Disemba Mosi 2023 katika maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya Sekondari ya Morogoro Mkoani Morogoro.
“Wadau wote muweke kipaumbele katika kundi hili la vijana ili kulinusuru na athari za UKIMWI na waweze kujitambua kwa kuwapa elimu waelewe madhara yake ili kusitokee tena maambuki mapya ya VVU kwa kuwa Serikali imejipanga kuutokomeza UKIMWI ifikapo 2030". Amesema Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu amesema kwa wale wote wanaoishi na VVU waendelee kutumia dawa za ARV kwa usahihi bila kuacha ili kufubaza VVU na kuimarisha Afya zao.
“Taifa linawategemea, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa huduma za ARV zinapatikana katika vituo vyote nchini vya kutolea huduma za Afya ili kila muhitaji aweze kupata huduma kwa urahisi". Amesema Waziri Mkuu.
Amesema kuwa Taasisi ya TACAIDS, Wizara ya Afya na wadau wote wa kudhibiti UKIMWI wametakiwa kubaini na kuyafanyia kazi maeneo yote ya gharama nafuu na yenye matokeo makubwa ili kuongeza bidii ya kutokomeza UKIMWI hapa nchini.
Mwisho, ametoa wito kwa wataalam kuendelea kutumia njia zote za mawasiliano ikiwemo magazeti, TV, Radio na mitandao ya kijamii kutoa elimu kuhusu VVU kwa lengo la kuleta mabadiliko ya tabia kwa Watanzania.