Customer Feedback Centre

Ministry of Health

USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA CANADA WAENDELEA KUIMARIKA

Posted on: July 20th, 2025

Na WAF - Dar es Salaam 


Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama leo Julai 20, 2025 amempokea na kumkaribisha Tanzania, Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada Mhe. Randeep Sarai pamoja na ujumbe aliyoambatana nao kutoka nchini Canada kwa lengo la kufanya ziara ya siku tano (5) nchini. 


Waziri Mhagama ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Canada kwa kuendelea kuisaidia Tanzania hasa katika Sekta ya Afya kwa mchango wanaoutoa kwenye mfuko wa pamoja wa afya (Health Basket Fund) kupitia mfumo wa ufadhili wa moja kwa moja katika vituo vya Afya awamu ya kwanza (2022–2027). 


"Lakini pia tunawashukuru sana kwa Msaada wa mradi wa afya ya uzazi na haki za vijana balehe, mradi wa kuboresha haki za wasichana kwa ajili ya afya bora Tanzania, mradi wa kuimarisha uuguzi wakati wa kujifungua ambao unalenga kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga kwa kuongeza upatikanaji wa wakunga wenye ujuzi," amesema Waziri Mhagama 


Aidha, Waziri Mhagama ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Canada katika sekta ya afya umeleta mafanikio mengi ikiwemo kupungua kwa vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka asilimia 67 mwaka 2015 hadi asilimia 43 mwaka 2022 kwa kila vizazi hai 1,000, kupungua kwa vifo vya akina mama wakati wa kujifungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai laki 100,000.


"Hata hivyo, tuna changamoto ya kupungua kwa vifo vya watoto wachanga, kutoka 25 kwa kila vizazi hai elfu 1,000 mwaka 2015 hadi 24 kwa kila vizazi hai elfu 1,000 mwaka 2022, hivyo basi, tunaiomba Serikali yako kuendelea kusaidia sekta ya afya ili kukabiliana na changamoto hii," amesema Waziri Mhagama